WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, akipata maelezo kutoka kwa Angela Shanira wa kitado cha tano sekondari ya Tusiime Tabata kuhusu masuala mbalimbali ya kisayansi kwenye maabara ya shule hiyo wakati Waziri alipofungua rasmi maabara ya kisasa ya sayansi na maktaba na mahafali ya tano ya kidato cha sita ya shule hiyo
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema serikali inaangalia iwezekano wa kuzipa ruzuku shule binafsi ili ziweze kujiendesha vizuri huku akizimwagia sifa shule za Tusiime kwa kuendelea kufanya vizuri kwa kutoa elimu bora na katika viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa.
Alitoa pongezi hizo leo alipozindua jengo la maabara za sayansi na maktaba ya shule hizo na mahafali ya tano ya kidato cha sita ambapo Membe alikuwa mgeni rasmi.
Alisema serikali imegundua umuhimu huo wa kuzipa ruzuku na imeanza kuliangalia upya suala hilo kwani litasaidia shule binafsi kupunguza ada hivyo watanzania wengi kupata fursa ya kupata elimu kwasababu gharama zinapopanda wazazi wamekuwa wakiumia.
Alisema nguvu ya uchumi wa gesi inaonyesha kuwa Tanzania itakuwa na uwezo wa kifedha wa kutoa ruzuku kwa shule binafsi kama ilivyo kwa baadhi ya nchi duniani ambapo shule hizo hupewa ruzuku ya hadi asilimia 40.
Vile vile, Waziri Membe alisema sifa za shule hiyo ndizo zimemvutia kwenda kujionea mwenyewe mambo mazuri ambayo amemekuwa akiyasikia huko nje kwa muda mrefu.
Alisema kwa maendeleo ya wanafunzi kitaaluma shuleni hapo ni ushahidi tosha wa dhamira ya dhati waliyonayo Tusiime kama taasisi ya kutoa elimu bora kwa vijana wa kitanzania kwani wamekuwa wakifanya vyema katika mitihani mbalimbali ya kimkoa, kikanda na kitaifa.
“Kweli nimejionea mwenyewe kwa macho yangu na nimeridhika kwamba sifa nzuri nazozisikia huko ni ukweli mtupu na mnastahili,” alisema Membe na kuongeza.
“Kwangu kama kiongozi mwandamizi wa serikali ya awamu ya nne, inanipa faraja kuona malengo na maazimio ya serikali ya kuhakikisha watoto wetu wanapata elimu na kujengewa maarifa na ujuzi vinatekelezwa kwa vitendo. Kwa namna ya pekee nawapongeza sana walimu kwa kufanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa katika kufundisha na kuwalea watoto hawa,” alisema Membe ambaye ni mwanadiplomasia aliyebobea na Mjumbe wa Kamati Kuu CCM.
Alisema kwa kutambua umuhimu wa elimu kwa maendeleo ya jamii, serikali itaendelea kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu na itaendelea kushirikiana na watanzania ambao wanatumia sehemu ya mali walizojaliwa na Mungu kuandaa mazingira ya kuwaelimisha wenzao.
Naye Mkuu wa shule ya sekondari Tusiime, Emil Rugambwa, alisema shule hiyo kama kawaida yake ni moja kati ya shule chache za binafsi zinazofanya vizuri zikiwa na idadi kubwa ya watahiniwa kulinganisha na shule zingine zinazofanya vizuri zikiwa na idadi ndogo ya Watahiniwa.
Alisema katika kuhakikisha Tusiime inatoa elimu bora na kukuza kiwango cha ufaulu, mafanikio yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka na hilo linathibitika kupitia wanafunzi waliohitimu kidato cha sita mwaka jana (2014) ambao idadi yao ilikuwa 256, idadi ambayo ni kubwa zaidi ukilinganisha na miaka iliyopita lakini wanafunzi wote walifaulu kati ya daraja I - III na kujiunga na vyuo Vikuu mbalimbali vya elimu ya juu ndani na nje ya nchi.
Vilevile, alisema mwaka 2014 shule ilikuwa na wanafunzi 208 wa kidato cha nne na wote wamefaulu mitihani yao kwa alama za juu kwa ufaulu wa daraja la kwanza, la pili na wachache walipata daraja la tatu na kwamba mafanikio hayo ndiyo yanayoifanya shule hiyo kukua kwa kasi.
“Kutokana na juhudi hizi za ndani ya shule tumejikuta tukienenda vema na kuzingatia mpango wa serikali wa “Matokeo makubwa sasa” (Big Result Now) maarufu kama BRN kwani shule ilishakuwa na mikakati na mipango yake ambayo kimsingi inatuweka katika nafasi nzuri ya kutekeleza na kupata matokeo makubwa sasa,” alisema Rugambwa.
|