Wednesday, 6 March 2013

HOTUBA YA DC WA HAI, KWENYE UFUNGUZI WA MKUTANO WA UMOJA WA WAKUU WA SHULE ZA SEKONDARI WILAYA YA HAI

HOTUBA YA MKUU WA WILAYA YA HAI,NOVATUS MAKUNGA KATIKA UFUNGUZI WA MKUTANO WA UMOJA WA WAKUU WA SHULE ZA SEKONDARI NCHINI(TAHOSSA)KWA WILAYA YA HAI KATIKA UKUMBI WA MOTEL PAPA MNAMO MACHI 6,2013.
·         Ndugu Mwenyekiti wa Umoja wa Wakuu wa shule za sekondari Tanzania[TAHOSSA] wilayani Hai,
·         Ndugu Viongozi wa TAHOSSA,
·         Ndugu Afisa Elimu wa wilaya,
      ·         Wakuu wote wa Shule za sekondari wilayani Hai.
Awali ya yote nianze kwa  kumshukuru mwenyezi Mungu kwa kutupa uzima na kutukutanisha hapa leo lakini pili kutuwezesha  kuendelea na kazi katika mwaka mpya wa 2013.
Kwa wale ambao hatujakutana  pamoja na kwamba huu ni mwezi Machi lakini kuna msemo wa kiingereza “Late better  than never”,hivyo basi  nitumie fursa hii kuwatakia mwaka mpya mwema wenye upendo na uwajibikaji.
Lakini jambo la pili nichukuwe fursa hii kuwashukuru kwa kunialika kuzungumza machache kwenye Mkutano huu  na niwapongeze waandaaji kwa kuweza kuwakutanisha wakuu wa shule za sekondari katika wilaya ya Hai.
Ingawa ni jumuiko la kawaida kwa kila mwaka lakini kupata idadi kubwa ni mafanikio makubwa hongereni sana.
Ndugu Mwenyekiti, Mkutano huu unafanyika katika kipindi hiki ambacho mjadala mkubwa hapa nchini ni matokeo ya kidato cha nne.Lakini Matokeo hayo ni hitimisho tu ya matokeo mengine ya darasa la saba na yale ya kidato cha pili.
Mnamo tarehe 18 Februari, 2013 Baraza la Mitihani la Taifa lilitangaza matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne ya mwaka 2012.  Wanafunzi 397,132 walifanya mtihani huo na kati ya hao, waliofaulu ni 126,851 yaani sawa na asilimia 34.5.  Wanafunzi 240,903 ambao ni sawa na asilimia 65.5 hawakufaulu mtihani huo.
Matokeo ya mitihani ya huo, yameshtua na kufadhaisha watu wengi nchini kwani hata shule zinazofahamika kuwa na historia ya kufaulisha vizuri kama vile seminari, shule za watu binafsi, za mashirika ya dini na sekondari kongwe za Serikali ambazo hazina matatizo kama ilivyo kwa zile sekondari za Kata, nazo safari hii hazikupata mafanikio kama ilivyo kawaida yao
Kwa upande wa wilaya ya Hai katika shule za serikali watahiniwa 1,688 wamefeli kabisa kwa kupata sifuri.Kwa upande wa ufaulu,wanafunzi wawili walifanikiwa kupata daraja la kwanza,wanafunzi watano daraja la pili,wanafunzi 44 daraja la tatu na wanafnzi 555 daraja la nne.
Kwa upande wa shule za binafsi,wao wamepata daraja la kwanza wanafunz 11,daraja la pili wanafunzi 44,daraja la tatu wanafunzi 111 na daraja la nne wanafunzi 405 ilhali waliofeli ni wanafunzi 145.
Kwa upande wa kidato cha pili ni vivyo hivyo,Wilaya ya Hai  imefanya vibaya kwa kupata wastani wa ufaulu wa asilimia 35 huku kiasi cha wanafunzi 940 wanalazimika kubakia katika kidato cha pili wakiwa miongoni mwa  wanafunzi 2,959 walifanya mtihani huo.
Ndugu mwenyekiti,Nyinyi mliopo hapa ni wadau nambari moja wa elimu katika wilaya yetu ya Hai na bahati nzuri mmekutana wakati  hivi sasa kila mmoja wetu yuko katika kuangalia tunafanya nini kuinusuru elimu yetu.
Uongozi wa serikali katika wilaya umeshapanga kuwa na mkutano na wadau wa elimukuzungumzia mikakati inayolenga kuinua hali ya elimu na kukomesha kabisa dosari zote ambazo zinasababisha elimu yetu kwenda chini ama kuzorota.
Ndugu mwenyekiti,mwezi uliopita nilikuwa na kundi la wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali wanaotoka wilaya ya Hai kupitia Umoja wa wanafunzi wanaosoma vyuo vikuu kutoka wilayani Hai[HAUSO] niliwaomba kwa kuwa wapo likizo basi wajitolee kufanyakazi za kuwafundisha wadogo zao walioko katika sekondari mbalimbali,hivyo walikubali na vijana  kumi na tano walikuwa huko katika shule.
Lakini mbali ya kufundisha niliwaomba wanafanyiye tathimini ya nini tunaweza kufanya katika kuhakikisha kuwa tunainua hali ya elimu katika wilaya yetu ya Hai.
Kwa sasa wote wamesharejea vyuoni lakini nilibahati kukaa nao na wamenieleza mengi ambayo wamyabaini katika shule zetu za sekondari na katika kuyashughulikia nimeona baadhi ni ya kuchukulia mkakati wa muda mfupi ama wa haraka.
Hivi sasa kuna vijana wetu ambao wana miezi michache sana kabla ya kuingia katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi na huu ukiwa ni mwezi machi na niliwauliza hao vijana vipi hali ipoje ? Nao walinijibu kwamba tusipochukuwa hatua matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka huu yanaweza kuwa mabaya maradufu ya matokeo ya mwaka jana.
Hivyo nyinyi mkiwa wakuu wa shule kwa taratibu za halali kabisa tuunganishe nguvu zetu katika kuchukuwa hatua za muda mfupi ambazo zitawasaidia vijana ambao wanajiandaa kufany mitihani ya kumaliza kidato cha nne wanafanya vizuri.
Kuna baadhi ya maeneo ambayo waliyaona na mengine pia yamo katika taarifa mbalimbali za wakaguzi wa elimu zinazofanyika kwa nyakati tofauti ambapo sisi kama wakuu wa shule tunaweza kujadiliana hapa na kuweka mkakati wa kuchukuwa hatua kwa lengo la kuwasaidia vijana wetu katika kujenga maisha.
Baadhi waliyoyaona vijana wetu wa vyuo vikuu ni pamoja na;
 1. Migogoro ndani ya ofisi za shule yaani Staff Room.
Katika mwezi mmoja wa kufanya kazi wamebaini kwamba katika baadhi ya shule kuna maelewano madogo ama hakuna kabisa kati ya mkuu wa shule na makamu mkuu wa shule pamoja na mwalimu wa taaluma.

2. Nidhamu ya mavazi kwa baadhi ya walimu.
Baadhi ya walimu wameondoka kabisa katika mazoea ambayo tuliyajenga miaka ya nyuma kwa katika jamii zetu walimu ni mfano wa kuigwa kwa kuingia katika mavazi yasiyokuwa ya staa yakiwemo ya kushusha suruali chini maarufu kama kata K na kuteremsha sketi chini.

3. Mtihani wa Mock kutokuwa na mfumo wa kuupima.
Mtihani huu haufanyiwi tathimini nzuri katika ngazi ya wilaya ili uweze kutumika katika kuwaandaa watahiniwa wanaotarajiwa kufanya mitihani ya kitaifa baada ya miezi michache mbeleni

4. Wanafunzi kushindwa kuelewa Lugha ya kufundishia.
Bado kuna tatizo kubwa kwa idadi kubwa ya wanafunzi wanaoanza kidato cha kwanza kuelewa vizuri lugha ya kujifunzia ya kiingereza kutokana na kutumia lugha ya Kiswahili kwa muda ya miaka saba katika shule za msingi.

5. Wanafunzi kuingia katika mahusiano ya Kimapenzi.
Imebainika kuwa baadhi ya wanafuni wanaingia katika uhusiano wa kimapenzi na hivyo kushindwa kujikitia katika masomo.

6. Wazazi kushindwa kutoa ushirikiano kwa walimu.
Baadhi ya wazazi wamekuwa na tabia ya kwenda shule kugombana na walimu mara walimu wanapochukuwa hatua za kuwarekebisha wanafunzi wanaopooka.

7. Baadhi ya mada za masomo hazifundishwi kabisa.
Imebainika kwamba baadhi ya topic katika masomo na hasa hisababti pamoja na masomo ya sayansi hazifundishwi kabisa mpaka wanafunzi wanamaliza elimu ya msingi

8. Kuingia kwa utandawazi na teknolojia ya kisasa.
Baadhi ya wanafunzi kutumia vibaya teknolojia ya kisasa hususani simu za mikononi na hivyo kujikita zaidi huko huku wakisahau jukumu lao kubwa ambalo ni kujifunza na kuelewa kile wanachojifunza.

Vijana hao walitoa baadhi ya mapendekezo yakiwemo ya mkakati wa muda mfupi wa kuwasaidia vijana wetu ambao wanatarajia kufanya mitihani yao mwaka huu ambayo ni pamoja na;

1. Kuwepo na utaratibu wa kubadilishana kufundisha baadhi ya
Topic miongoni mwa walimu kwa walimu wa shule za jirani kwa maana wa shule moja kwenda shule nyingine kutegemeana na umahiri wake katika topic husika.

2. Kuongeza saa za kuwafundisha kidato cha nne.
Wanafunzi wote wanaotarajia kufanya mitihani ya kidato cha nne waweze kuwahi kufika shuleni saa moja asubuhi na baadaye warudi tena jioni baada ya kutoka shule saa nane na nusu mchana

3. Kuandaliwa kisaikolojia.
Kutokana na matokeo ya mitihani iliyopita kuwa mabaya basi kwa vyovyote vile hali hiyo inaweza kuwaathiri baadhi ya watahiniwa watarajiwa na hivyo ni vyema ukaandaliwa mfumo wa kuwajenga kisaikolojia.

4. Mkazo katika kufundishwa mbinu za kufanya mitihani.
Ratiba ya kufundishwa jinsi ya mbinu za kufanya mitihani imekuwa fupi na hivyo ni vyema walimu katika shule wakaangalia mkakati wa kuwafundisha wanafunzi mbinu za kufanya mitihani

5. Uimarisha wa bodi za shule.
Kuimarisha ama kufufua bdi za shule baada ya kubainika kwamba shule nyingi katika wilaya ya Hai hazina kabisa bodi za shule ama zilizopo zinashindwa kuwajibika.Kuwepo kwa bodi hizo kutaimarisha mahusiano kati walimu na wazazi na kuweka mkakati wa pamoja na kuwasaidia wanafunzi.

6. Mpango wa kuwapa motisha walimu wanaofanya vizuri.
Kwa walimu ambao watafanikiwa kuwezesha idadi kubwa ya wanafunzi kufanya vizuri kwa kupata alama za juu za A ama B,basi kuwe na utaratibu wa kuwazawadia na kutambua mchango wao katika elimu.

Ndugu mwenyekiti,Haya ni baadhi tu ya mapendekezo ya muda mfupi ambayo nyinyi kama wana taaluma na wadau namba moja mnaweza kuyajadili na kuyatengenezea mapendekezo kwa ajili ya kuchukuwa hatua katika muda muafaka.

Mapendekezo mengine ni ya muda wa kati na mrefu ambayo tutayatengezea utaratibu baada ya kumaliza mchakato wa kukutana na wadau pamoja na makundi mbalimbali ambayo kwa namna moja yanahusika katika masuala ya elimu.

Wilaya inawategemea sana katika kuirejesha katika hadhi ya miaka ya nyuma kama miongoni mwa wilaya ambazo zilikuwa na wasomi katika miaka ya awali mara tua baada ya uhuru mwaka 1961

Ndugu mwenyekiti baada ya masuala ya elimu ambayo hasa ndiyo jukumu lenu kubwa kama wakuu wa shule za sekondari,naomba mniruhusu kuongelea baadhi ya masuala ya kijamii kutokana na nyinyi mbali ya kuwa wakuu wa shule lakini pia ni sehemu ya jamii na pia wengi wenu katika jamii mnanafasi kubwa ya kukubaliwa na kuheshimika sana.

1. Kukithiri kwa tabia ya unywaji wa pombe ikiwemo pombe haramu ya gongo

Ndugu Mwenyekiti,sote tunafahamu vijana tunaowafundisha ni sehemu ya kundi kubwa la vijana katika wilaya yetu ambalo sasa hivi linaendelea kuangamia kutokana na kukithiri kwa unywaji wa pombe ikiwemo pombe haramu ya gongo.

Kwa mwananchi yeyote mwenye uchungu na wilaya yetu ya Hai lazima suala hili litamgusa kwani hivi sasa ni janga la wilaya na hali hii ikiendelea baada ya miaka mitano mpaka kumi ijayo hatutakuwa tena na kizazi kilichoandaliwa vyema kupambana na changamoto za maisha.

Lakini baya zaidi baadhi ya viongozi wenzetu katika vijiji na vitongoji wamekuwa vinara katika kuhakikisha biashara hii ya pombe haramu ya gongo inaendelea kudumu.

Rai yangu kwenu ni kushirikiana katika kuhakikisha kwamba tunaweka mkakati wa kupambana na watengenezaji,wauzaji na watumiaji wa pombe haramu ya gongo na kuhakikisha imekwisha kabisa.

Lakini mbali na pombe haramu ya gongo lakni kuna tatizo kubwa la matumizi ya pombe halali kwa muda kwa idadi kubwa ya vijana zikiwemo zile zinazobebeka kirahisi ndani ya mifuko ya plastki pamoja na pombe yetu ya asli ya mbege.

Pamoja na kuwepo kwa sheria ambayo hivi sasa tumeanza kuitekeleza kwa nguvu zote lakini nyinyi kwa upande wenu naomba niwaombe kwa nafasi zenu kuendelea kuelimisha jamii athari za kunywa pombe kwa saa ishirini na nne ndani ya siku saba za wiki katika siku thelathini za mwezi.

Sisi kwa upande wetu tutaendelea kusimamia sheria ya saa za unywaji wa pombe ambapo ni saa tisa jioni mpaka saa tatu usiku kwa siku za katikati ya wiki na saa nne kwa mwisho wa wiki kwa maana jumamosi na jumapili.

2. Utunzaji wa mazingira

Ndugu Mwenyekiti,mazingira ndiyo uhai wetu.Kwa kutambua hilo na kasi kubwa iliyojitokeza ya ukataji wa miti,serikali katika mkoa wa kilimanjaro kwa nia nzuri kabisa ilisitisha vibali vya ukataji wa miti kwa ajili ya mbao na magogo.

Maamuzi haya hayakuchukuliwa kwa ajili ya manufaa ya mtu binafsi au kwa lengo la kuwakomoa wananchi,bali kuthamini ustawi wa maisha ya  jamii yote ya mkoa wa Kilimanjao wakiwemo wakazi wa wilaya ya Hai.

Babu zetu walifanyakazi kubwa ya kupanda miti kwa kasi na ndiyo maana wengi wetu wakati tunazaliwa tulikuta wilaya ya Hai ikiwa na mazingira ya kuvutia yenye mvua za kutosha zilizotusaidia kuendesha shughuli zetu za kilimo na ufugaji kwa ufanisi mkubwa.

Kibaya kilichojitokeza hivi sasa bila ya kuthamini jitihada za wazazi wetu za kupanda miti na kuitunza hivi sasa tumekuwa tukikata miti hii kwa kasi kubwa sana na kuharibu mazingira hali ambayo imesababisha hata msimu wa mvua usiwe wa uhakika huku joto likiongezeka maradufu.

Kutokana na hali hiyo ndipo serikali mkoani Kilimanjaro ikachukuwa maamuzi magumu ya kusitisha vibali vya ukataji wa miti kwa ajili ya mbao na magogo.

Ndugu mwenyekiti,cha kushangaza katika maeneo mengi ya wilaya ya Hai bado kuna baadhi ya vinara wa ukataji wa miti miongoni mwao ni viongozi wenzetu.

Wanaofanya vitendo hivi wanafahamika hivyo ombi langu la pili kwenu ni kuomba ushirikiano wenu katika kuwafichuwa wanaofanya hivyo kwa kuwasiliana name moja kwa moja lakini pia kuendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kuendelea kutunza mazingira.

Lakini sanjari na hilo hivi sasa tupo katika kampeni ya upandaji wa miti katika maeneo mbalimbali.
Tumeagiza na kuwaandikia kama wakuu wa shule kuanzisha kitalu ama bustani ya miche ili msimu wa mvua utakapoamza basi tusipate tatizo la miche.

Kama wakuu wa shule hakikisheni mnakwenda kusimamia zoezi la maandalizi ya upandaji wa miti kwa kuwa na vitalu vya miche vya ya kutosha kwa maana mvua zitapoanza kunyesha basi tuanze mara moja zoezi la upandaji wa miti.


1. Utawala bora

Ndugu Mwenyekiti,Changamoto ya masuala yenye mwelekeo wa utawala bora limekuwa tatizo kubwa sana katika wilaya yetu kuanzia sisi tulioko ngazi ya wilaya mpaka viongozi wetu walioko katika ngazi za vijiji.

Aidha Uwajibikaji limekuwa tatizo kubwa sana likitugusa sisi viongozi wa kisiasa mpaka wataalamu wetu wa ngazi mbalimbali huku tatizo kubwa likiwa kusahau majukumu yetu.


Kwa upande wa changamoto hii nitaieleza katika maeneo mawili tu ambayo sisi kama wakuu wa shule na wanajamii katika maeneo yetu tunaweza kusaidia kwa kiasi cha juu sana.

Changamoto ya kwanza inahusu ufanyikaji wa vikao vya kisheria katika ngazi za vijiji na kata.Hilo limekuwa tatizo kubwa sana katika wilaya yetu.Kila unapita katika vijiji malalamiko makubwa ni ufanyikaji wa mikutano ya vijiji na hasa ajenda inayohusu kusomwa kwa taarifa ya mapato na matumizi.

Kwa uchache sana pia tuna tatizo la ufanyikaji wa mikutano ya kamati za maendeleo za kata yaani WDC katika baadhi ya kata.

Changamoto hizo zote siyo siri zinafahamika vizuri kwa maofisa wetu wa ngazi za tarafa na kata hususani kwa ufanyikaji wa mikutano mikuu ya kijiji na kwa ile ya ngazi ya kata zinafahamika katika halmashauri yetu ya wilaya.

Sasa tunalenga kumaliza tatizo la ufanyikaji wa vikao vya kisheria katika ngazi ya vijiji.Mkiwa wakuu wa shule mnanafasi kubwa ya kushauri na kuelimisha pia kama wasomi hivyo nawaombeni ratiba za vikao vya kisheria katika vijiji vyenu zinafanyika vikiwa na ajenda zote muhimu,mahudhurio na maamuzi.

Lakini kwa upande wa masuala ya utawala bora nimalizie kwa kuwataka nyinyi wakuu wa shule kutojitenga na miradi mbalimbali na badala yake kuhakikisha mnafuatilia kwa ukaribu miradi yote inayotekelezwa katika maeneo yenu iwe ndani ya shule ama katika ngazi ya vijiji.

Naomba nimalize kwa kuwashukuru tena kwa kunipa heshima kubwa ya kunialika katika mkutano wenu huu ambao umenipa fursa kubwa ya kuzungumza nanyi kwa mapana kuhusiana na masuala ya elimu nnchi kwa ujumla pamoja na katika wilaya ya Hai

Nawatakia mafanikio katika mkutano wenu,Mungu ibariki wilaya ya Hai,Mungu ibariki Tanzania, asanteni kwa kunisikiliza

No comments:

Post a Comment