MKATABA WA MUUNGANO
Baina ya
JAMHURI YA TANGANYIKA
Na
JAMHURI YA WATU WA ZANZIBAR
Kwa kuwa Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar
zinafahamu uhusiano wa muda mrefu watu wake na mshikamano na kukuza
uhusiano huo na kuimarisha mshikamano na kukuza umoja wa watu wa Afrika,
zimekutana na kutafakari Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya
watu wa Zanzibar.
Na kwa kuwa Serikali za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa
Zanzibar, zinapendelea ya kwamba Jamhuri hizi mbili ziungane kuwa Jamhuri
moja huru moja kwa amasharti ya makubaliano yafuatayo:
Kwa hiyo IMEKUBALIWA baina ya Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika na ya
Jamhuri ya watu wa Zanzibar kama ifuatavyo:-
(i) Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar zitaungana na kuwa
Jamhuri huru moja.
ii) Katika kipindi cha kuanza kwa Muungano mpaka Baraza la Kutunga katiba
lililotajwa katika ibara ya (vii) litakapokutana na kupitisha katiba ya
Jamhuri ya Muungano (Kuanzia hapa kitaitwa kipindi cha mpito), Jamhuri ya
Muungano itaongozwa kwa masharti ya ibara ya (iii) mpaka ya (vi).
(iii) Katika kipindi cha mpito katiba ya Jamhuri ya Muungano itakuwa katiba
ya Tanganyika iliyorekebishwa ili kuweka:
a) Chombo tofauti cha kutunga sheria na Serikali kwa ajili ya Zanzibar kwa
mujibu wa sheria zilizopo za Zanzibar na vitakuwa na mamlaka ya mwisho
katika Zanzibar kwa mambo yote isipokuwa yale tu yaliyo chini ya bunge na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano;
b) Nafasi ya makamo wawili wa Rais mmoja kati yao akiwa ni mkaazi wa
Zanzibar atakuwa ndiye kiongozi wa Serikali iliyotajwa kwa ajili ya
Zanzibar na atakuwa ndiye msaidizi mkuu wa rais wa Jamhuri ya Muungano
katika utekelezaji wa kazi za Serikali kwa upande wa Zanzibar;
c) Uwakilishi wa Zanzibar katika bunge la Jamhuri ya Muungano;
d) Mambo mengine yatayofaa au kuhitajika ili kuipa nguvu Jamhuri ya
Muungano na mkataba huu.
(iv) Mambo yafuatayo yatakuwa chini ya bunge na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano:-
a) Katiba na Serikali ya Jamhuri ya Muungano
b) Mambo ya nchi za nje
c) Ulinzi
d) Polisi
e) Mamlaka yanayohusika na hali ya hatari
f) Uraia
g) Uhamiaji
h) Mikopo na biashara ya nchi za nje
i) Utumishi katika Jamhuri ya Muungano.
j) Kodi ya mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika, ushuru wa
forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa nchini na kusimamiwa na idara
ya forodha
k) Bandari, mambo yanayohusu usafiri wa anga, Posta na Simu
v) Bunge na Serikali vilivyotajwa vitakuwa na mamlaka ya mwisho juu ya
mambo yote yahusuyo Jamhuri ya Muungano na kuongezea mamlaka juu ya mambo
yote yahusuyo Tanganyika.
Sheria zote zilizopo za Tanganyika na za Zanzibar zitaendelea kutumika
katika maeneo yao bila kuathiri:-
a) Masharti yoyote yatakayowekwa na chombo chenye mamlaka ya kutunga sheria.
b) Masharti yatakayowekwa kwa amri ya Rais wa Zanzibar juu ya sheria yoyote
inayohusu jambo lolote lililotajwa kwenye ibara ya (iv), na kufuta sheria
yoyote inayolingana Zanzibar.
c) Mabadiliko yoyote kama yataonekana yanafaa au kuhitajika ili kufanikisha
Muungano na mkataba huu.
(vi) (a) Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano atakuwa ni Mwalimu J. K.
Nyerere na ataongoza Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa kufuata masharti
ya mkataba hu na kwa kusaidiwa na maofisa wengine atakaowateuwa toka
Tanganyika na Zanzibar na watumishi wa Serikali zao.
b) Makamo wa kwanza wa Rais kutoka Zanzibar aliyeteuliwa kwa kufuata
marekebisho kama yalivyoelezwa na ibara ya 3, atakuwa Sheikh Abeid Karume.
(vii) Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kukubaliana na Makamo wa Rais ambaye
ni kiongozi wa serikali ya Zanzibar
a) Atateua tume kwa ajili ya kutoa mapendekezo kwa ajili ya katiba ya
Jamhuri ya Muungano.
b) Ataitisha Baraza la kutunga katiba ikiwa na wawakilishi kutoka
Tanganyika na Zanzibar katika idadi itakayoamuliwa likutane katika kipindi
cha mwaka mmoja tokea kuanza kwa muungano kwa madhumuni ya
kutafakarimapendeke zo ya tume iliyotajwa juu na kupitisha katiba ya Jamhuri
ya Muungano.
(viii) Mkataba huu utahitaji kuthibitishwa kwa kutungiwa sheria na Bunge la
Tanganyika na Baraza la Mapinduzi la Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kwa
kushirikiana na Baraza lake la Mawaziri, na mkataba kupitishwa na kuundwa
kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano na ya Zanzibar kwa kufuata masharti
yaliyokubaliwa.
KWA KUSHUHUDIA HAPA Julius K. Nyerere, Rais wa Jamhuri ya Tanganyika na
abeid Karume, Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, wametia saini nakala
mbili za mkataba huu, hapa Zanzibar siku ya tarehe Ishirini na mbili ya
mwezi Aprili, 1964.
____________ _________ ______
Umepitishwa katika Bunge siku ya tarehe Ishirini na Tano ya Aprili, 1964.
P. MSEKWA
…………………..Karani wa Bunge
Nathibitisha kwamba Muswada wa Sheria hii ulipitishwa na Bunge kwa mujibu
wa ibara ya 35 ya katiba.
A.S. MKWAWA
……….………………………..Spika
No comments:
Post a Comment