Wananchi
sasa kutuma maoni kuhusu Katiba Mpya kwa ‘sms’
Oktoba 31, 2012
Na Mwandishi Wetu, DSM
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetangaza namba nne (04) za simu za
mkononi ambazo wananchi kwa sasa wanaweza kuzitumia kutuma ujumbe mfupi
wa maandishi (‘sms’) kutoa maoni yao kuhusu Katiba Mpya.
Kwa mujibu wa taarifa ya Tume hiyo kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo
(Jumatano, Oktoba 31, 2012) namba ambazo wananchi wanaweza kutuma maoni
yao kwa njia ya ‘sms’ ni 0715 (Tigo) /0767 (Vodacom) / 0787 (Airtel) /
0774 (Zantel) – 08 15 08.
“Kwa kuzingatia kuwa Watanzania wengi waliopo mijini na vijijini
wanamiliki simu za mkononi, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inaamini kuwa
njia hii ni fursa nyingine muhimu kwa Watanzania kuweza kuwasilisha
maoni yao kwa Tume,”
imesema sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa na
Katibu wa Tume hiyo Bw. Assaa Rashid.
Ili kutuma maoni, Bw. Assaa amesema, mwananchi anapaswa kufungua ukurasa
wa kutuma ujumbe mfupi wa maandishi (sms) katika simu yake na kuandika
maoni yake pamoja na jina lake kamili, jinsia, mahali anapoishi, umri,
elimu na kazi na kutuma kwenda kwenye namba yoyote kati ya zilizotolewa.
Kwa mujibu wa Bw. Assaa, baada ya kutumwa, maoni hayo yatakwenda kwa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambapo yatafanyiwa kazi pamoja na maoni
yanayokusanywa kwa njia nyingine.
Uanzishwaji wa njia hii ya ujumbe mfupi wa maandishi unalenga kuwapa
fursa nyingine wananchi kutoa maoni yao. Tume ya Mabadiliko ya Katiba
pia inapokea maoni ya wananchi kupitia mikutano ya ana kwa ana; barua
pepe (maoni@katiba.go.tz); njia za posta (S.L.P. 1681, Dar es Salaam au
S.L.P. 2775, Zanzibar); ukurasa wa ‘facebook’ (Tume ya Mabadiliko ya
Katiba) na tovuti (http://www.katiba.go.tz/).
Katika taarifa yake hiyo, Tume imewaomba wananchi kutumia namba hizo
kutuma maoni yao binafsi kuhusu Katiba Mpya bila kushawishiwa na watu,
makundi, vyama au taasisi yoyote na kufafanua kuwa Tume inatarajia
kuanza kupokea maoni ya makundi, vyama na taasisi mara baada ya kumaliza
kukusanya maoni binafsi ya wananchi katika awamu ya nne na ya mwisho
itakayomalizika mwezi Desemba, 2012.
No comments:
Post a Comment