Tuesday 15 January 2013

JAMAL MALINZI KUCHUKUA FOMU YA KUGOMBEA URAIS TFF LEO

Na Mwandishi wetu

JAMAL Emil Malinzi, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Kagera (KRFA), anatarajiwa kuchukua fomu ya kugombea Urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) leo mchana, makao makuu ya shirikisho hilo, Ilala mjini Dar es Salaam.  
 
Habari ambazo BLOGU hii imezipata kutoka kwa watu wa karibu wa Katibu huyo wa zamani wa klabu ya Yanga, zimesema kwamba Malinzi atachukua fomu mchana wa leo.
 
Katika uchaguzi uliopita wa TFF uliofanyika Desemba 14, mwaka 2008, Malinzi alikuwa mpinzani mkuu wa rais anayemaliza muda wake, Leodegar Chillah Tenga ambaye amekwishatangaza hagombei tena. 
 
Katika uchaguzi huo, uliofanyika kwenye ukumbi wa NSSF Water Front, Dar es Salaam, Tenga alishinda kwa kura 64 kwa 39.
 
Awali, Malinzi alienguliwa kwa kigezo cha uzoefu, lakini akarejeshwa kuwania nafasi hiyo baada ya kushinda rufaa yake.
 
Katika uchaguzi huo ulioshuhudiwa na Mwakilishi wa FIFA, Ashford Mamelodi, Athumani Nyamlani alishinda nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, baada ya kujikusanyia kura 65 kati ya kura 107 zilizopigwa na kura mbili kuharibika, akimshinda Lawrence Mwalusako aliyepata kura 39 na Ali Mwanakatwe aliyeambulia kura moja.
 
Nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais, ambayo kwa sasa imefutwa, ilikwenda kwa Ramadhani Nassib aliyemwangusha mpinzani wake wa karibu, Damas Ndumbaro aliyepata kura 45.
 
Hadi sasa, mbali na Malinzi mgombea mwingine anayetarajiwa katika nafasi ya Urais ni Athumani Nyamlani, Makamu wa kwanza wa sasa wa Rais wa TFF.
Jumla ya watu 26 hadi jana walikuwa wamekwishachukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali, kuelekea uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Februari 24, mwaka huu.
 
Hata hivyo, idadi hiyo ni kwa wale wanaochukua fomu hizo katika ofisi za TFF, kwani vilevile zinapatikana kupitia tovuti ya TFF ya www.tff.or.tz ambapo mwisho wa kuchukua na kurejesha ni saa 10 kamili alasiri Januari 18 mwaka huu.
Waliochukua jana ni Michael Wambura anayewania umakamu wa rais wakati kwa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni Mbasha Matutu, Muhsin Balhabou, Salum Chama, Titus Osoro na Zafarani Damoder.
 
Idadi kamili ya waliochukua ni Michael Wambura, Ramadhan Nassib na Wallace Karia (Makamu wa Rais). Kwa upande wa wajumbe na kanda zao kwenye mabano ni Salum Chama (Kagera na Geita), Mugisha Galibona, Samuel Nyalla, Titus Osoro na Vedastus Lufano (Mara na Mwanza).
 
Epaphra Swai na Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu), Charles Mugondo, Elly Mbise na Twahili Njoki (Arusha na Manyara), Yusuph Kitumbo (Kigoma na Tabora), Ayubu Nyaulingo, Nazarius Kilungeja na Selemani Kameya (Katavi na Rukwa) na James Mhagama (Njombe na Ruvuma).
 
Athuman Kambi (Lindi na Mtwara), Hussein Mwamba na Stewart Masima (Dodoma na Singida), Farid Nahdi (Morogoro na Pwani), Khalid Mohamed (Kilimanjaro na Tanga) na Muhsin Balhabou, Shaffih Dauda na Zafarani Damoder (Dar es Salaam).
Mwenyekiti wa soka wa Kagera, Jamal Malinzi kushoto katika picha ya pamoja na Rais wa TFF anayeng'atuka katika nafasi hiyo Leodigar Tenga
 
Naye Said Mohamed amechukua fomu ya kuwania umakamu mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board).

No comments:

Post a Comment