Tuesday 8 January 2013

Tunaajiri walimu 28,000 mwezi huu – Rais Kikwete

 

  • Tunaajiri walimu 28,000 mwezi huu – Rais Kikwete
  • 14,600 wa Msingi; 14,060 wa Sekondari na 80 Vyuo vya Ualimu

SERIKALI itaajiri na kusambaza walimu 28,746 katika shule za msingi na sekondari kuanzia mwezi huu wa Januari 2013, hatua ambayo itapunguza kwa zaidi ya nusu ukosefu wa walimu katika shule za Serikali nchini.

Mpaka sasa Tanzania ina upungufu wa walimu 57,177 katika shule za Serikali, tatizo ambalo Serikali inasema kuwa italimaliza katika miaka michache ijayo kutokana na idadi kubwa ya walimu wanaofundishwa katika vyuo mbali mbali nchini.

Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametangaza mjini Igunga mchana wa jana, Jumatatu, Januari 7, 2013 kuwa kati ya walimu hao watakaoajiriwa na kusambazwa 14,600 watakuwa wa shule za msingi, walimu 14,060 watakuwa wa shule za sekondari na 80 watakuwa walimu wa vyuo vya ualimu.

Akihutubia maelfu ya wananchi wa mjini Igunga kwenye Uwanja wa Barafu kwenye siku ya pili ya ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Tabora, Rais Kikwete amesema kuwa mikoa yenye uhaba mkubwa zaidi wa walimu ndiyo itapewa kipaumbele katika mgawo huo wa walimu.

Mkoa wa Tabora ni moja ya mikoa yenye uhaba mkubwa wa walimu, ikiwa na ukosefu wa walimu 2, 055 na Wilaya ya Igunga pekee ikiwa inahitaji kiasi cha walimu 285.

Hii itakuwa mara ya pili mfululizo kwa Serikali kuajiri na kusambaza idadi kubwa ya walimu wa shule za msingi na sekondari katika jitihada za kumaliza tatizo la ukosefu wa walimu nchini ambalo kwa namna moja linachangia matatizo ya elimu nchini.
Mwaka juzi, Serikali iliajiri na kusambaza walimu 24,621 ambao kati yao 11,379 walikuwa wa shule za msingi, walimu 13,246 walikuwa wa shule za sekondari na walimu 42 walikuwa ni wa vyuo vya elimu.

Wakati shule za Serikali nchini zinaendelea kukabiliwa na upungufu wa walimu, shule binafsi nchini zina ziada ya walimu, shule za msingi zikiwa na ziada ya walimu 2, 857 na zile za sekondari zikiwa na ziada ya walimu 459 hali inajionyesha katika matokeo mazuri ya mitihani kwa wanafunzi wa shule hizo.

Rais Kikwete amewaambia wananchi kuwa Serikali pia inakabiliana ipasavyo na matatizo mengine yanayoikabili sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na ukosefu wa maabara, ukosefu wa nyumba za kutosha za walimu na ukosefu wa vitabu vya wanafunzi.

Rais Kikwete pia amezungumzia suala la huduma ya maji nchini akisema kuwa Serikali yake imeonyesha jitihada za kukabiliana na ukosefu wa maji katika maeneo mbali mbali ya Tanzania.

Kwa upande wa Igunga, Rais Kikwete amesema kuwa kufuatia kuzinduliwa kwa Mradi wa Maji wa Bulenya asubuhi ya leo, mji wa Igunga na vijiji vitatu vinavyozunguka mji huo sasa vinapata maji kwa asilimia 70.

Ameahidi kuwa asilimia 30 iliyobakia itapatiwa majawabu na mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria ambayo yatavutwa kwa ajili ya matumizi ya wakazi wa miji ya Nzega, Igunga na Tabora na vijiji ambako mabomba ya mradi huo yatapitia.

Rais Kikwete ambaye aliwasili Mkoani Tabora juzi, jana mchana ameondoka Igunga kuanza ziara ya Wilaya ya Nzega.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.

8 Januari, 2013

No comments:

Post a Comment