Wednesday 31 October 2012

TANAPA YAHAMISHA, YATEUA WAKURUGENZI WAPYA

Na Seif Mangwangi, Arusha.

SHIRIKA la hifadhi za Taifa nchini (TANAPA) kupitia bodi yake ya   udhamini, imefanya mabadiliko ya nafasi za kazi kwa baadhi ya  watumishi wake kwa kuteua wakurugenzi wapya wawili na kuwahamisha
wengine vituo vya kazi.

Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari jana  Afisa uhusiano wa  Tanapa Paschal Shelutete, nafasi zilizofanyiwa mabadiliko ni pamoja na  nafasi mbili za wakurugenzi wa idara na wakuu wanne wa hifadhi za
Taifa.

Wakurugenzi walioteuliwa ni pamoja na  Martine Loibooki ambaye anakuwa  Mkurugenzi  wa Uhifadhi makao makuu ya shirika mjini Arusha,kabla ya hapo alikuwa mkuu wa hifadhi ya Tarangire, Witness Shoo anayekuwa mkurugenzi wa  utumishi na utawala, kabla ya uteuzi huo alikuwa mkurugenzi msaidizi
kwenye mfuko wa millennia (Millenium Challenge Account).

Wakuu wa hifadhi waliohamishwa vituo vya kazi ni pamoja na Steven Qolli anayetoka Ruaha kwenda Tarangire,Wiliam Mwakilema aliyekuwa  hifadhi ya Mikumi anakwenda Serengeti na Noelia Myonga kutoka Gombe  kwenda Kitulo.

Mabadiliko hayo pia yamewagusa baadhi ya watumishi waliokuwa makao  makuu ya shirika ambapo Christopher Timbuka kutoka makao makuu  ameteuliwa kuwa mkuu mpya wa hifadhi ya taifa Ruaha.

Akizungumzia lengo la kufanya mabadiliko hayo Shelutete alisema  ni  zoezi la kawaida ndani ya shirika hilo lengo kuu likiwa ni kuongeza  utoaji wa huduma na ufanisi wa majukumu ya kila siku ya shirika hilo.

“Mabadiliko ni ya kawaida na yamelenga kuongeza ufanisi na kuongeza  ubora wa huduma zetu na si vinginevyo, kwa kuwa hifadhi zetu zote zina   hadhi sawa hakuna ambayo ni muhimu kuzidi nyingine” alisema.

wakati huo huo aliwataka watumishi wa shirika hilo kutangaza utalii wa ndani ili kuvutia watanzania wengi kutembelea hifadhi za Taifa ili kuliongezea shirika mapato yatokanayo na watalii wa ndani.

“Kwa muda mrefu mapato ya shirika yametokana na watalii wanaotoka nje  ya nchi lakini sasa tumewaelekeza watumishi na hasa wakuu wa hifadhi kutangaza utalii wa ndani ili wananchi wapate fursa ya kuzitembelea hifadhi za taifa”

Kuhusu ujangili na uwindaji haramu, Shelutete alisema kuwa shirika hilo limeongeza nguvu kubwa katika doria zake ili kupunguza au kutokomeza kabisa ujangili.

“Tumewaambia wakuu wa hifadhi pamoja na kutangaza utalii wa ndani lakini pia wahakikishe kuwa wanapambana kwa nguvu zote na ujangili na wawindaji haramu”

No comments:

Post a Comment