Wednesday 14 November 2012

CHIKAWE: WAJUMBE WA TUME YA KATIBA TUMIENI MAJAJI



ARUSHA

WAZIRI wa katiba na sheria Mathias Chikawe ameitaka tume ya mabadiliko ya katiba kuwatumia kikamilifu Majaji,mahakimu,Mawakili na wanasheria kote nchini katika mchakato wa mabadiliko ya katiba kwakua ni watumiaji wakubwa wa katiba ya sasa.

Chikawe ametoa changamoto hiyo leo alipokua akifungua warsha ya siku moja inayoendelea katika hoteli ya kitalii ya Snow Crest jijini Arusha ya umuhimu wa katiba katika utoaji wa haki katika vyombo vya maamuzi ikiwemo mahakama.

Warsha hiyo ambayo imeungana na mkutano wa mwaka wa majaji na mahakimu wa mahakama zote hapa nchini ukiwa na lengo la kutazama namna haki inavyoweza kupatikana na kwa wakati katika vyombo mbalimbali vya kutafsiri sheria za nchi.

Waziri Chikawe alisema mchango wa majaji,mahakimu na mawakili unatokana na ukweli kwamba kundi hilo linatafsiri za kuzibadili kila siku sheria mbalimbali za nchi zinazotokana na katiba hali ambayo inaweza kutoa mchango mkubwa kwa tume hiyo ya mabadiliko ya katiba ya  nchi.

“hili kundi ni muhimu sana kwakua wao ndiyo kazi yao kila siku wanapotoa hukumu au utetezi wanatafsiri sheria ambazo nyingi zipo ndani ya katiba ambayo ndiyo sheria mama baada ya kuziona kama zina mapungufu ikiwemo kupitwa na wakati”alisema Chikawe.

Hata hivyo Chikawe alisema kwasasa wizara yake imejipanga kikamilifu katika kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati bila kucheleweshwa ikiwa ni kwa kuboresha uendeshaji wa mashauri mbalimbali yaliyopo katika mahakama zote nchini.

Alisema uboreshaji huo ni pamoja na kuachana na matumizi ya majaji na mahakimu kuandika mashauri kwa kutumia mkono na badala yake waanze kutumia njia mbadala zikiwemo za kielektroniki ili kurahisisha kazi zao.

Alisema kufanikiwa kuondokana na teknolojia hiyo ya kizamani kutawezesha kupunguza msongamano wa mashauri katika mahakama hapa nchini ambapo wananchi wengi hufikia hatua ya kukosa imani na chombo hicho na kutafuta njia za mkato katika kutafuta haki zao ambazo ni pamoja na kutoa rushwa.

Hata hivyo aliahidi kufanyiwa kazi kwa marekebisho mbalimbali ya sheria No.4 ya mwaka 2012 ambayo inataka kutenganishwa kwa shughuli za kimahakama na za kiutendaji wa serikali,kuanzishwa kwa mfuko wa mahakama pamoja na kurejeshwa kwa uwajibikaji wa watumishi kwa kuwaweka chini ya idara ya mahakama.

Pia aliwataka wakuu wa vyombo hivyo kuwa wakali kwa wale wote wanaoonekana kuichafua sekta hiyo kwa kufanya kazi kinyume na maadili ikiwa ni pamoja na kuwafukuza kazi pasipo kuwaonea haya ili kubaki na wale wanaofanya kazi hiyo kwa wito kama inavyotakiwa.

Mkutano pamoja na warsha hiyo inahudhuriwa na viongozi wa ngazi zote za mahakama kutoka Tanzania bara na Zanzibar pamoja na nchi jirani ikiwemo Kenya kwaajili ya kubadilishana uzoefu wa masuala ya kisheria.

No comments:

Post a Comment