Wednesday 14 November 2012

JAJI WARIOBA KUVIVAMIA VYAMA VYA SIASA



Arusha 

MWENYEKITI wa tume ya mabadiliko ya katiba nchini Jaji Joseph Warioba amesema watavivamia vyama vyote vya siasa na taasisi zilizowalisha maneno wananchi katika maoni ya katiba ili watoe ufafanuzi baada ya kubaini wananchi hao kukosa maelezo ya kutosheleza juu ya hoja hizo ambapo waliwachonganisha na tume hiyo baaba ya kuwataja.

Jaji Warioba alieleza hayo leo alipokua akizungumza na vyombo vya habari katika katika hoteli ya kitalii ya Snow Crest Jijini Arusha alipokua akihudhuria warsha ya siku moja ya umuhimu wa katiba mpya katika utoaji wa haki katika vyombo mbalimbali vya maamuzi zikiwemo mahakama inayoendelea katika hoteli hiyo ya Snow Crest Jijini Arusha.

Jaji Warioba alisema kuwa katika maeneo mbalimbali tume yake ilikopita imekuta wananchi wengi wakitoa maoni mbalimbali yanayofanana na pindi wanapotakiwa kutoa ufafanuzi wake wamekuwa wakishindwa hali inayowapa wakati mgumu katika kuyafanyia kazi maoni yao.

Alisema baada ya kukutana na mazingira hayo waliwahoji wananchi hao walipopata maoni hayo ambapo wote walivitaja baadhi ya vyama vya siasa na taasisi mbalimbali zilizowaandalia waraka huo ili watoe maoni hayo.

Jaji Warioba alisema vyama baadhi ya siasa,CCM hakipo vimeandaa baadhi ya waraka huo na kuwapatia wananchi pamoja na taasisi mbalimbali zikiwemo za Kidini pamoja na zile za Kijamii.

Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo imesababisha ugumu wa zoezi hali ambayo iliwasababisha kuweka azimio kuwa mara baada ya kumaliza maeneo hayo watazifuata taasisi na vyama hivyo vya siasa ili kuvihoji undani wa hoja hizo ili kupata ufafanuzi wa kutosha kufanyia kazi.

“sisi tutavifuata vyama hivyo pamoja na taasisi hizo maana ziliwalisha wananchi maneno lakini wananchi hao hao wanashindwa kuzifafanua au kuzitolea maelezo hoja zao kitu kinachoonyesha waliandaliwa waraka huo na watu hao”alisema Warioba.

Hata hivyo Jaji Warioba alisema ili kubaini kuwa hoja walizoshindwa kuzitolea maelezo au ufafanuzi walilishwa na vyama vya siasa na taasisi hizo ni pale ambapo wananchi hao hutolea maelezo na ufafanuzi hoja mbalimbali ambazo zinaonekana ni zao wenyewe.

“yani ukiwasikiliza katika baadhi ya hoja ambazo hawajalishwa na vyama vya siasa au taasisi kwa maslahi yao unajua kabisa maana hoja zao wanaweza kuzitolea ufafanuzi barbara kwahiyo tutawafuata wenye hoja zao ili watupe ufafanuzi”alisema Jaji Warioba.

Aidha Warioba alieleza kuwa kwa kiwango kikubwa uvamizi wa zoezi hilo uliokuwa umefanywa na vyama vya siasa na taasisi kwa maslahi yao binafsi umepungua baada kwasasa wananchi wengi wamekuwa wakitoa maoni yao ya hoja zinazowahusu wao tofauti na wakati zoezi hilo lilipokua linaanza.

Alisema hadi hivi sasa jumla ya wananchi wapatao elfu hamsini wametoa maoni yao kwa kuzungumza katika mikutano inayoitishwa na tume yake,wengine zaidi ya elfu 87 wametoa maoni yao kwa njia ya maandishi huku wengine wengi wakitoa maoni yao kwa njia za mitandaa ya kijamii na vyombo vya habari ambao kwa ujumla wake wanafikia zaidi ya laki tisa ambayo tayari wameshayakusanya.

Hata hivyo Jaji Warioba alitoa changamoto kubwa inayowakabili kwa sasa ni muda wa miezi kumi na minane waliyopewa ya kukamilisha kazi hiyo ambayo wanaiona kuwa haitatosheleza na kutahadharisha kuwa upo uwezekano mkubwa wa kuomba kuongezewa muda wa kazi hiyo kwakua kanuni zinaruhusu.

Mwisho.



No comments:

Post a Comment