Friday 23 November 2012

RC ARUSHA: WAKAZI KUWENI TAYARI KUPOKEA MAENDELEO





RC ARUSHA: WAKAZI KUWENI TAYARI KUPOKEA MAENDELEO 

MKUU wa mkoa wa Arusha Magessa Mulongo amewataka wakazi wa jiji la Arusha kujiweka tayari kuendana na maendeleo yanayojitokeza ikiwemo uwepo wa taasisi mbalimbali za kimataifa jiji hapo.

Mulongo amesema hayo leo alipokua akizungumza na vyombo vya habari kuhusu uzinduzi wa jingo la kisasa la makao makuu ya jumuiya ya Afrika Mashariki unaotarajiwa kufanyika mnamo Novemba 28 mwaka huu.

Alisema kuwepo kwa makao hayo makuu ya jumuiya hiyo kunaendana sambamba na ongezeko la watu watakaokua watumishi wa jumuiya hiyo kutoka nchi mbalimbali ambao watahitaji pia malazi yaliyo bora pamoja na mahitaji mengine mengi.

Kufuatia kauli hiyo aliwataka wakazi hao kuboresha majengo yao yaliyo jirani na maeneo ya mijini ili yaendane na kasi hiyo pamoja na ukarabati mkubwa uliofanywa na serikali kama hatua za mapokezi ya ujio huo wa jumuiya hiyo.

Katika hatua nyingine Mulongo alisema maandalizi yote ya uzinduzi wa jingo hilo yamekamilika na kinachosubiriwa na ujio wa Marais wote wan chi zinazounda jumuiya hiyo watakaokutana mkoani Arusha.

Mulongo alisema mara baada ya kukamilika kwa shughuli hiyo viongozi hao wataondoka mkoani hapa kuelekea jijini Nairobi nchini Kenya ambapo watahudhuria kongamano la kujadili masuala mbalimbali yahusuyo muungano huo.

Hata hivyo viongozi hao wakiwa nchini Kenya watafanya shughuli ya uzinduzi wa barabara kuu ya Afrika Mashariki kutokea Tanzania hadi Nairobi nchini Kenya ambayo kwa upande wa Tanzania tayari jiwe la msingi la ujenzi huo lilishawekwa.

Akizungumzia mikakati ya mkoa wa Arusha katika kuboresha mazingira na kuwa katika hali nzuri alisema tayari ofisi yake imeshawaelekeza viongozi wa jiji la Arusha kuandaa mipango miji mizuri ikiwa ni pamoja na utaratibu mzuri wa ujenzi.

Alisema mkakati huo utawakumba baadhi ya watu ambao watapaswa kufidiwa kupisha uboreshaji huo na kwamba kwasasa mpango madhubuti unaandaliwa ili kuwezesha kupatikana kwa fedha zitakazotumika kuwafidia wahanga hao.

Pia alisema katika kuhakikisha msongamano wa magari unaondoka katika maeneo ya kati ya jiji tayari mkakati umekamilika wa upanuzi wa barabara kuu ya Moshi-Arusha ili kuwezesha kutembea magari manne kwa wakati mmoja kuanzia eneo la Mianzini hadi Tengeru mradi unaofadhiliwa na fedha za mfuko wa jumuiya ya Afrika Mashariki.

Pia alisema mpango mwingine ni ule wa ujenzi wa barabara mpya ya mzunguko kutoka eneo la Ngaramtoni hadi uwanja wa ndege wa Arusha kazi inayofanywa na serikali ya Tanzania na hatimaye awamu ya pili ni kuunganisha barabara hiyo hadi eneo la Tengeru ambapo ukikamilika utawezesha kuondoa msongamano huo kwakua mtu hatakua na haja ya kuingia mjini kama ana safari ya nje ya mji.



No comments:

Post a Comment