Friday 23 November 2012

WIZARA YA KILIMO NA CHAKULA YASHINDWA KULIPA MAMILIONI VIBARUA WAKE



WIZARA YA KILIMO NA CHAKULA YASHINDWA KULIPA MAMILIONI VIBARUA WAKE

WIZARA ya Kilimo, Chakula na Ushirika inadaiwa kushidwa kulipa Mamilioni ya fedha za Vibarua  wanaofanya kazi katika Kituo cha kueneza Teknolojia za Kilimo ATTC, cha kanda ya Kaskazini kilicho Themi jijini Arusha kwa miezi sita sasa.

Vibarua hao Saba  wamesema hawajalipwa madai yao tangia Mwezi marchi mwaka huu hadi sasa na hivyo wameonyesha wasi wasi kuwa huenda fedha hizo ambazo zimetengwa kwa ajili ya malipo yao zimechachuliwa  hali inayowafanya wao waishi katika mazingira magumu na kwa matumaini kama wagonjwa wa Ukimwi ambao wajui lini watapona.

Vibarua hao wakizungumza na vyombo vya habari katika ofisi za Idara habari maelezo, mkoa wa Arusha, wamesema kuwa hawajalipwa Ujira wao tangia mwezi Marchi mwaka huu hivyo wao wanashindwa kulipia kodi za nyumba, kugharimia matunzo ya familia ,kugharimia matibabu .

Wamesema kuwa wanajipanga kukifanyia uharibifu mkubwa katika   kituo hicho kutokana na kutolipwa ujira wao kwani wamevumilia lakini sasa uzalendo umewashinda.

Kutokana na Wizara hiyo  kushindwa kuwalipa kiasi cha shilingi milioni 4,200,000, wanazodai tangia Marchi hadi Novemba mwaka huu, wanaona kuwa hawatendewi haki na kuna uwezekano fungu hilo limechakachuliwa ,na wajanja wa wizara hiyo wasiokitakia kituo hicho mafanikio katika maonyesho ya kila mwaka ya Nane nane.

Kituo hicho kilianzishwa na wizara hiyo mwaka 2008 na kiliingia mkataba na vibarua hao kwa ajili ya kuendesha Vishamba vidogo vidogo vya mafunzo ya mazao mbalimbali ya kilimo kwa kipindi chote cha mwaka. Hivyo wakapendekeza Kituo hicho kifungwe kwa sababu wamechoka kufanya kazi bila kulipwa kwa wakati.

”Inashangaza kila tukitaka kulipwa lazima twende kwenye vyombo vya habari vinginevyo hatulipwi hali hii itaendelea mpaka lini ni bora kituo hiki kifungwe vinginevyo tutafanya uharibifu mkubwa  ”, walisema vibarua hao.

Vibarua hao wamekuwa wakifanya kazi ya kuhudumia vipando vya mazao mbalimbali yakiwemo mazao ya mizizi ,migomba, vikolezo na miti ya matunda.

Vibarua hao wamekuwa wakitoa mafunzo endelevu kwa mwaka mzima kwa watu mbalimbali wanaotembelea kituo hicho kwa kutumia teknolojia na mbinu zitakazowawezesha wakulima kulima kilimo chenye  tija na kupata faida kubwa

Vibarua hao wamesema wanashangazwa na hatua ya Wizara hiyo kuingia mkataba na kampuni binafsi ya Ulinzi ya SGS,kulinda Kituo hicho  ,ambayo imekuwa inalipwa kila mwezi ,lakini wao hawalipwi .

Wamesema kuwa wao wanafanya kazi kubwa ya kutunza vipando,na na wao ndio husababisha Wizara hiyo kupata ushindi kila mwaka katika maonyesho hayo ya Nane nane lakini hawathaminiwi  licha ya mchango mkubwa wanaoutoa wa kutunza vipando hivyo.

Msimamizi wa kituo hicho, Elias Ernest, alipoulizwa kuhusiana na madai hayo alikiri na kueleza kuwa ameshawasilisha Wizarani
 .
Ameongeza  kuwa Vibarua hao wamekuwa wakitumia lugha za vitisho ikiwa ni kushinikiza walipwe madai yao pia wamepoteza moyo wa kufanya kazi .


No comments:

Post a Comment