Friday 14 December 2012

DC HAI ATOA SIKU 14 WALIVAMIA MSITU NA KUKATA MITI KWENYE VYANZO VYA MAJI KUONDOKA

  Ukataji wa mito katika maeneo ya vyanzo vya maji kunakofanywa na watu waliovamia maeneo hayo

Uharibifu mkubwa wa ukataji wa kandokando ya mito katika wilaya ya Hai
 Na MWANDISHI MAALUM, HAI
Mkuu wa wilaya ya Hai, Novatus Makunga ametoa muda wa siku kumi na nne kwa watu wote waliovamia vyanzo vya maji katika eneo la Shirinjoro wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wawe wameondoka kwa hiari yao wenyewe.

Waandishi wa habari waliotembelea vyanzo hivyo wamekuta uzio mkubwa wa tofali ukiendelea kujengwa katika moja ya vyanzo hivi huku eneo lingine likiwa na nguzo za uzio wa waya


Mkuu huyo wa wilaya ametoa agizo hilo katika mkutano wa kijiji cha Shirinjoro aliohitisha baada ya kutembelea vyanzo vitatu vya maji na kubaini kwamba kuna uvamizi mkubwa wa shughuli za kibinadamu ndani ya maeneo hayo ambayo yanalindwa na  sheria ya mazingira.

Alisema kuwa baada ya muda huo kupita sheria itachukiwa mkondo kwa wote ambao watakaidi kwa makusudi kuondoka katika maeneo hayo ambao yanalindwa kwa mujibu wa sheria ya mazingira.


Vyanzo hivyo ni pamoja na Njoro juu,chemchemu ya Kiladeda na chanzo cha maji cha Kitifu.

Makunga ameeleza kuwa vyanzo hivyo vitatu ni muhimu kwa matumizi ya maji ya wananchi wa wilaya ya Hai pamoja na manispaa ya Moshi na kwamba vinalindwa na sheria ya mazingira na vilishatamkwa katika gazeti la serikali.


Aliwapongeza wananchi kwa kufichua uvamizi wa hivi karibuni wa wananchi wawili ambao walikuwa mbioni kuanza kujenga uzio katika vyanzo hivyo ambavyo alieleza historia inaonyesha vilianza kulindwa na viongozi wa kabla la Kichagga wanaofahamika kama Mangi.


"Ningewashanga sana endapo mngenyamazia uvamizi huu wa vyanzo vya maji ambavyo viliweza kulindwa na wazee wenu na viongozi wa wakati huo yaani Mangi,endeleeni kuvichua kila vitendo vya uharibifu wa mazingira sisi tupo saa ishirini na nne kuwatumikia,"alisema.

 
Aidha mkuu huyo wa wilaya ya Hai aliiagiza halmashauri ya wilaya ya Hai kuhakikisha inaweka mawe yanayoonyesha maeneo yasiyoruhusiwa kufanya shughuli za kibinadamu katika vyanzo hivyo vitatu pamoja na vyanzo vingine vilivyopo katika wilaya hiyo.


Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliushtumu uongozi wa kijiji hicho kwa madai ya kuhusika na kuuza maeneo ya vyanzo hivyo vya maji hatua ambayo walilazimu kupeleka malalamiko kwa mkuu wa wilaya aliyeingilia kati na kuzuia ujenzi wa uzio kuzunguka moja ya chanzo hicho.


Hata hivyo baadhi ya wananchi waliomba kupewa muda zaidi kwa madai ya kwamba walikuwa hawafahamu kwamba hivyo ni vyanzo vya maji ambavyo vinalindwa kisheria.


Awali afisa mazingira katika halmashauri ya wilaya ya Hai,Mathew Ntilicha ameueleza mkutano huo kwamba jumla ya watu thelathini na saba wamevamia vyanzo hivyo kwa kujenga ndani ya mita thelathini kutoka pembezoni mwa vyanzo hivyo na wanapashwa kuondoka katika kipindi hicho.


Ameeleza kuwa kuanzia leo wataaanza kupita katika maeneo hayo yote kuweka alama katika nyumba zote ambazo imeingia katika eneo la vyanzo hivyo vya maji.


Ntiliacha ameeleza kuwa vyanzo hivyo vilitambuliwa rasmi kupitia gazeti la serikali mnamo mwaka 2005 na hivyo kulindwa kisheria.


       
-           

No comments:

Post a Comment