Thursday 27 December 2012

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Singida alumbana na diwani wa viti maalum (CCM) kuhusiana na ripoti ya Sikika.





Dk.Henry Mmbando,wa ofisi ya mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Singida akitoa ufafanuzi juu ya tuhuma zilizotolewa na shirika la Sikika juu ya uwajibikaji katika kutoa huduma katika halmashauri hiyo.(Picha na Nathaniel Limu).

 Mwanakamati wa shirika lisilo la kiserikali la Sikika, diwani (CCM) Salima Kundya akimtuhumu diwani wa mkutano huo diwani Elia Digha (hayupo pichani) kwa kauli yake kuwa kamati ya Sikika haijui kitu chochote kuhusu na utoaji wa huduma ya afya katika halmashauri ya wilaya ya Singida. Salima alikuwa akitoa tuhuma hizo mbele ya mkutano wa mrejesho wa taarifa ya uwajibikaji katika utoaji wa huduma za afya iliyokuwa ikitolewa na shirika la Sikika
Na Nathaniel Limu.
Halmashauri ya wilaya ya Singida imesema haitakubali kuchonganishwa na wananchi wake na vyombo au taasisi yakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), kwa kutoa taarifa zisizofanyiwa utafiti wa kina.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Alli Juma, amesema hayo muda mfupi kabla ya mkutano wa mrejesho wa ripoti/taarifa ya shirika lisilo la kiserikali la Sikika lenye makazi yake jijini Dar-es-salaam, iliyohusu ufuatiliaji wa uwajibikaji katika utoaji wa huduma za afya, haujafungwa rasmi.
Amesema taarifa iliyotolewa na shirika la Sikika, kwa kiasi kikubwa haikufanyiwa utafiti wa kina, kitendo ambacho kinaweza kusababisha halmashauri kutokuelewana vizuri na wananchi wake.
Alli ambaye ni Afisa Utumishi amesema Sikika hawakuwa na mawasiliano wala ushirikiano mzuri na wakuu wa idara katika kupata ukweli wa taarifa mbalimbali walizokuwa wanazikusanya.
“Mimi niwaombeni tu ndugu zangu wa Sikika, fanyeni kazi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu, halafu mkiandika mabaya, upande wa pili andikeni pia mazuri hata kama yapo machahe”,alisema Alli.
Mkutano huo uliokuwa chini ya uenyekiti wa diwani (CCM) Elia Digha, Mwenyekiti huyo alitoa shutuma nzito kwamba wafanyakazi wa Sikika na kamati nzima iliyofuatilia uwajibikaji wa huduma za afya, haijui lolote.
“Mimi nasema timu yote iliyoleta taarifa hii, haijui lolote, naomba siku za usoni tushirikiane vizuri katika kufuatilia uwajibikaji katika sekta zote, kutoa taarifa za jumla jumla kama hii, mtaacha watu waichukie bure serikali”, alisema Digha ambaye ni diwani wa kata ya Msange jimbo la Singida Kaskazini.
Baada ya maneno hayo mazito, diwani wa viti maalum (CCM) Salima Kundya, aliyeshiriki na Sikika kufuatilia uwajibikaji katika sekta ya afya, alimtolea uvivu Mwenyekiti Digha, kuwa lengo lake ni kutaka kuficha ukweli uliopo kwenye taarifa hiyo.
“Kama sisi madiwani wawili wa CCM mliotuchagua tukashirikiane na Sikika na tukabaini yote yaliyopo kwenye taarifa ya Sikika kuwa ni ya ukweli mtupu, halafu wewe unasema hatujui lo lote, basi wewe mwenyekiti Digha na madiwani wote wa CCM walioshiriki kutachagua na ninyi wote hamjui kitu au cho chote kinachofanyika ndani ya halmashauri hii”, alisema Salima huku uso wake ukionyesha kujawa na hasira.
Baada ya maneno hayo ya diwani Salima, bila kulazimishwa, Digha ambaye pia ni msaidizi wa mbunge wa jimbo la Singida kaskazini Lazaro Nyalandu, alisimama na kuomba radhi kwa matamshi yake ambayo yalilenga kuidhalilisha kamati iliyoambatana na Sikika.
Katika mengi yaliyomo kwenye taarifa ya Sikika, kuna hoja iliyotolewa na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali, inaonyesha kuwa halmashauri hiyo ilikuwa na shilingi bilioni 1,686,561,960 za miradi mbalimbali ya maendeleo.
Lakini taarifa hiyo, ilionyesha kiasi cha shilingi bilioni 1.6 sawa na aslimia 61.4,hazikutumika kwa wakati, kitendo hicho kinamaanisha kuwa baadhi ya miradi ya maendeleo, ilikamilika nusu ama haijakamilika kabisa.

No comments:

Post a Comment