Thursday 6 December 2012

WAZIRI UMMY AZINDUA KAMPENI KUPINGA UNYANYASAJI WA KIJINSIA

Na:  Usu-Emma Sindila na Sakina Mfinanga
NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu, ameahidi kuwa atahakikisha vinapatikana vituo maalum vya kuripoti taarifa za unyanyasaji na matusi katika masoko na magulio wilaya ya Ilala ili kurahisisha mapambano dhidi ya unyanyasaji.

Ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kampeni za siku 16 kupinga unyanyasaji kijinsia katika soko la Kivukoni Feri leo iliyobebwa na kauli mbiu ya “pinga unyanyasaji na matusi sokoni” “nipe riziki na si matusi” iliyozinduliwa katika masoko matano ya Ilala, Kigogo Saambusa, Kibasila, Mchikichini na Feri.

Amesema kuwa, kutokana na hali halisi, wanawake wanapaswa kutoa taarifa katika madawati maalum katika vituo vya polisi, lakini kutokana na umbali wa vituo hivyo anaangalia uwezekano wa kusogeza huduma hizo kwenye masoko hayo.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Equality for Growth (EfG), Jane Magigita, ameeleza kuwa, katika tafiti zilizofanywa zinaonyesha kuwa asilimia 43 ya wanawake wamejikita katika ujasiriamali katika sekta isiyo rasmi ambapo wanakabiliwa na changamoto kadha wa kadha ikiwemo mitaji midogo, maeneo madogo ya kufanyia biashara wakijihusisha na biashara kama za mama ntilie, ushonaji, kutengeneza batiki na nyinginezo.

Ameongeza kuwa, utafiti uliofanywa katika masoko 10 ya jijini Dar es Salaam unaonyesha kuwa wanawake wamekuwa wakikabiliwa na matatizo ya unyanyasaji ukatili wa kingono, matusi na kiuchumi.


Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu, akitoa hotuba wakati wa uzinduzi wa kampeni ya pinga unyanyasaji na matusi sokoni iliyofanyika Soko la Kivukoni, Ferri Jijini Dar es Salaam ikiwa ni muendelezo wa siku 16 za kupinga unyanyasaji kijinsia.

Naibu Waziri Ummy Mwalimu na Balozi wa Uingereza nchini Diana Croner, wakikata utepe kuzindua mabango yatakayobandikwa katika masoko mbalimbali yakihamashisha kupinga vita dhidi ya unyanyasaji kijinsia na matusi sokoni.
Aidha ameeleza kuwa, kampeni hii inatarajiwa kufikishwa katika masoko yote Jijini Dar na baadaye nchi nzima ili kuleta mwamko miongoni mwa watumiaji wa masoko.

No comments:

Post a Comment