Friday 21 December 2012

WAFANYAKAZI WA VODA WACHANGIA MILIONI 50 YATIMA

Ni msaada kwa ajili ya kampeni yake ya ‘Pamoja na Vodacom msimu huu wa sikukuu

Wakati maandalizi ya msimu huu wa sikukuu yakizidi kushika kasi, Kampeni ya ‘Pamoja na Vodacom’ bado inaendeleza ziara zake, ambapo kwa mwezi huu Kampeni hiyo imetenga zaidi ya shilingi milioni 50 kwa lengo la kuwafikia watoto yatima nchi nzima. Kampeni ya Pamoja na Vodacom, inayoendeshwa chini ya Mfuko wa Vodacom Foundation, awali ilijulikana kama Care and Share Kampeni, kabla ya kubadilishwa hivi karibuni.

Mfuko wa kusaidia Jamii wa Vodacom, kama sehemu ya mwendelezo wa harakati zake za kuhakikisha inasogea karibu zaidi kwa jamii, kwa mwezi huu, itaungana na wafanyakazi wengine katika idara zote ndani ya Kampuni hiyo kwa kuchangia vifaa mbalimbali, vikiwemo vyakula, fedha na mavazi kwa watoto yatima sehemu mbalimbali nchini. Mkuu wa Mfuko wa Kusaidia Jamii wa Vodacom, (Vodacom Foundation) Yessaya Mwakifulefule, alisema michango yote kwa mwezi huu imetokana na moyo wa kujitoa na namna wafanyakazi wa kampuni hiyo wanavyoguswa na watoto yatima waliopo kwenye vituo mbalimbali vya malezi nchini.

“Tumetenga zaidi ya milioni 50 kwa ajili ya kusaidia watoto yatima msimu huu wa sikukuu, ambapo kati ya fedha hizo kila idara ndani ya Kampuni ya Vodacom imechangia kima cha chini cha shilingi milioni 3,” alisema Mwakifulefule.

Na kuongeza kuwa mbali ya mchango huo, kila mfanyakazi kwa nafasi yake atapata fursa ya kuchangia“Mwishoni mwa wiki hii, tutatembelea Kituo cha watoto yatima cha Don Bosco kilichopo Kimara, ambapo wafanyakazi wa idara yetu ya Huduma kwa Wateja, watatoa msaada wa vifaa vya usafi, mashuka, foronya na vyakula, na baadaye tutatembelea mikoani,” alisema Mwakifulefule.

Kampeni ya pamoja na vodacom ni fursa pekee na kiungo muhimu chini ya Vodacom Foundation, katika kuhakikisha masuala muhimu yakiwemo mahitaji ya watoto yatima yanafikiwa na kupatiwa ufumbuzi kwa maslahi yao.



Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, mamia ya maisha ya watoto yatima nchini yamebadilishwa na kuwa bora kupitia kampeni hiyo, ambayo inaratibiwa na Mfuko huo, na kupitia michango ya wafanyakazi wake.

No comments:

Post a Comment