“Alikua mfano dhahiri wa neno mtanashati”-Zawadi Machibya, mratibu wa msiba na mtangazaji wa BBC
Swahili
Na: Freddy Macha
Kanisa la St Annes Lutheran katikati ya jiji la London juzi Jumamosi
lilikuwa kituo maalum cha kumwaga na kuwa wasifu wa maisha ya marehemu Freddy Alex Mtoi aliyekuwa
mtangazaji wa BBC Swahili kwa miaka mingi.
Ibada hiyo iliyoendeshwa na wachungaji
Tumaini Kalaghe na Mathew Jutta, ilihudhuriwa na wanahabari mbalimbali
kutoka BBC , Ofisa wa Ubalozi wa Tanzania, Clement Kiondo, marafiki wa karibu
waliomjua marehemu na wanananchi wa sehemu toka Tanzania, Afrika na Ulaya.
Mratibu wa mazishi , Zawadi Machibya, ambaye ni mtangazaji wa BBC, aliendesha shughuli na kuwajulisha wasemaji
wote waliozungumzia kwa kuanza kueleza namna neno “mtanashati” lilivyomvaa
Freddy Mtoi aliyefariki usiku wa kuamkia Jumamosi tarehe 17 Novemba, 2012.
Mchungaji Mathew Jutta alikumbusha kwamba safari yetu wanadamu huanzia kwa
Mungu na kuishia kwa Mungu. Akailinganisha
nsafari hiyo na ile ya kutoka nyumbani Afrika kuja Majuu (ambapo paliitwa Mtoni
enzi mchungaji alipokuja Ulaya takribani miaka 20 iliyopita). “Kwa wanaobakia
ni huzuni lakini kwa anayesafiri ni furaha yenye matumaini.” Akimzungumzia marehemu alitaka zaidi
kututuliza roho tuliyobakia.
Maneno haya yalisimama dede kama dhamira kuu ya msiba. Kwamba badala ya
kuhuzunika tujiratayarishe tunakokwenda kwa kuzingatia maneno ya Biblia, Yohana
Mtakatifu 3:20 : “ Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji
kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa.”
Wafanyakazi wenzake marehemu Mtoi nao waliendeleza hoja kwa kutueleza undani wa bidii yake marehemu kazini, tabia
yake ya uungwana na upole. Akifafanua kwa kina, mtangazaji wa BBC toka Kenya Solomon Mugera alitoa mfano
namna marehemu alipokuwa tayari kumenyeka hata wakati wenzake wakitaka
kupumzika kama wakati wa sikukuu ya Krismasi.
Mugera :“ Marehemu hakuwa mlalamishi au mbishi. Alikua haogopi kufanya
kitu ambacho hakifahamu.”
Akitoa maelezo katika lugha ya Kiswahili na Kiingereza kwa niaba ya wageni
wengine, Solomon alitaja mfano mwingine mkubwa wa jinsi Mtoi alivyokua mchapa kazi
asiyenung’unika kiasi ambacho hata alipokuwa mgonjwa aliwaambia wenzake “ni
kitu kidogo tu” wasitie shaka, kumbe mwenzetu alikua akielekea katika kifo.
Salim Kikeke mtangazaji gwiji aliyefanya kazi na marehemu toka Bongo miaka
kumi iiliyopita alitukumbusha zaidi kwa undani vipindi Freddy Mtoi alivyovitoa
kwa kuacha sauti yake isikike kwa wastani wa dakika moja.
Hapo tulimsikia
akiwahoji wananchi mbalimbali mitaani Uingereza. Mfano kipindi alichowauliza watu maana ya mti wa Krismasi, unaothaminiwa sana na Wazungu.
Kati ya wahojiwa alikuwa mchungaji
Tumaini Kallaghe aliyeongoza sala hii juzi.
Tulipata vile vile fursa ya kusikiliza sauti za wazazi wake Mtoi wakieleza
namna alivyokuwa mtoto mwenye bidii, mtiifu na aliyeanza kuipenda kazi ya
uanahabari toka angali mdogo sana.
Mbali na wafanyakazi walikuwepo pia marafiki zake wa karibu , mathalan
Prochest Tairo aliyefuta dhana iliyoenea ( toka msiba ulipotokea) kwamba
marehemu alikuwa msiri na mtu wa kujificha.
Tairo ambaye pia ni bloga na alimjua Mtoi toka wakisoma wote sheria chuo kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1997- 2002 alisema:
“Kwa nje alikuwa akionekana mkimya sana, mkiongea anasikiliza anatabasamu.
Lakini ukishamzoea ni mzungumzaji sana...si kweli alikuwa mkimya, ila ilibidi
akuzoee.”
Aliongeza kueleza marehemu alipenda mazoezi ya viungo. Siku moja walikuwa
mahali hadi ikafika usiku sana, lakini marehemu alitaka awahi Gym afanye
angalau mazoezi nusu saa kabla ya kuelekea nyumbani. Wengi hatukujua alikuwa
mpenda mazoezi.
Ibada iliendelea kwa nyimbo, sala na wahudhuriaji kutoa heshima zetu za
mwisho mbele ya jeneza, kabla ya kusafirishwa Dar es Salaam, leo Jumatatu.
Idhaa ya BBC Swahili ambayo ilihusika sana na matayarisho haya ikisaidiana
na Israel Saria, mwanahabari wa michezo anayeendesha tovuti ya Tanzania Sports,
iliwakilishwa na watangazaji wengi maarufu wakiwemo pia Charles Hillary, Idi
Sefu, Zuhura Yunus na Peter Musembi.
Akitoa neno lake Israel Saria alisema alijuana na Freddy Mtoi toka
Tanzania. Saria ataisindikiza maiti inayotarajiwa kuwasili Dar es Salaam Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, kwa ndege ya British Airways, Jumanne saa
moja asubuhi.
Mipango ya Ibada na mazishi Tanzania itafanyika nyumbani kwa wazazi wake Tabata Maduka Manne jijini Dar es Salaam, saa Saba mchana Jumatano.
Mazishi yatafanyika makaburi ya Kinondoni ,
Jumatano hiyo hiyo saa tisa alasiri.
Habari zaidi tembelea:
No comments:
Post a Comment