Na: Usu-Emma Sindila na Sakina
Mfinanga
NAIBU Waziri wa Maendeleo ya
Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu, ameahidi kuwa atahakikisha vinapatikana
vituo maalum vya kuripoti taarifa za unyanyasaji na matusi katika masoko na
magulio wilaya ya Ilala ili kurahisisha mapambano dhidi ya unyanyasaji.
Ameyasema hayo wakati wa
uzinduzi wa kampeni za siku 16 kupinga unyanyasaji kijinsia katika soko la
Kivukoni Feri leo iliyobebwa na kauli mbiu ya “pinga unyanyasaji na matusi
sokoni” “nipe riziki na si matusi” iliyozinduliwa katika masoko matano ya
Ilala, Kigogo Saambusa, Kibasila, Mchikichini na Feri.
Amesema kuwa, kutokana na hali
halisi, wanawake wanapaswa kutoa taarifa katika madawati maalum katika vituo
vya polisi, lakini kutokana na umbali wa vituo hivyo anaangalia uwezekano wa
kusogeza huduma hizo kwenye masoko hayo.
Akizungumza katika uzinduzi
huo, Mkurugenzi wa Equality for Growth (EfG), Jane Magigita, ameeleza kuwa,
katika tafiti zilizofanywa zinaonyesha kuwa asilimia 43 ya wanawake wamejikita
katika ujasiriamali katika sekta isiyo rasmi ambapo wanakabiliwa na changamoto
kadha wa kadha ikiwemo mitaji midogo, maeneo madogo ya kufanyia biashara
wakijihusisha na biashara kama za mama ntilie, ushonaji, kutengeneza batiki na
nyinginezo.
Ameongeza kuwa, utafiti
uliofanywa katika masoko 10 ya jijini Dar es Salaam unaonyesha kuwa wanawake
wamekuwa wakikabiliwa na matatizo ya unyanyasaji ukatili wa kingono, matusi na
kiuchumi.
Aidha ameeleza kuwa, kampeni
hii inatarajiwa kufikishwa katika masoko yote Jijini Dar na baadaye nchi nzima
ili kuleta mwamko miongoni mwa watumiaji wa masoko.
No comments:
Post a Comment