Ø Nyuki waleta
kizazaa msibani
Ø Ni baada ya
usia wa marehemu kupuuzwa.
NA SEIF MANGWANGI, MOSHI
MWENYEKITI wa
Halmashauri wa Wilaya ya Moshi Vijijini, Morris Makoyi juzi alilazimika
kuongoza mamia ya waombolezaji kutimua mbio kuokoa roho zao baada ya kushambuliwa
na kundi la nyuki waliovamia msiban.
Tukio hilo la aina yake, na lisilo la kawaida
lilitokea baada ya kuzikwa kwa marehemu Agnes Malya(30) ambaye inasemekana
aliacha usia kuwa kusiwe na mbwembwe kama vile
vyakula, pombe, suti na sare zingine katika mazishi yake.
Katika mbio hizo za
kuokoa maisha baada ya kundi kubwa la nyuki kuvamia mwishoni mwa msiba huo,
Makoyi akiongozana na Paroko wa Parokia ya Mkombole aliyefahamika kwa jina moja
la Ephraim waliacha magari ya kifahari waliyofika nayo msibani na kukimbilia
mgombani.
Nyuki hao wakiwa
katika makundi makubwa matano walijitokeza na kuanza kuwashambulia waombolezaji
hao mara baada ya mazishi ya marehemu Agnes Malya (30) aliyezikwa katika Kijiji
cha Osaki Wilaya ya Moshi vijijini.
Tukio hilo ambalo si
la kawaida linahusishwa na madai ya kupuuzwa kwa usia wa marehemu ambaye
alipinga kuandaliwa kwa vyakula na vinywaji vitu ambavyo vitagharimu fedha
ambazo zingetosha kugharamia matibabu yake kutokana ugonjwa wa kansa ya ziwa uliogharimu
maisha yake .
Kutokana na kizaazaa
hicho chakula na vinywaji vyenye thamani
ya zaidi ya shilingi milioni tano vinasemekana
vilimwagwa kama ishara ya kutimiza alichokisema marehemu Agnes . Lakini hilo
lilifanyika baada ya nyuki kuwakumbusha waombolezaji juu ya usia wa marehemu.
Kutokana na tukio
hilo,baadhi ya waombolezaji walikimbizwa katika vituo vya afya vilivyo karibu
na kijiji hicho akiwamo wifi wa marehemu
ambaye inasemekana ndiye aliyeandaa
chakula katika msiba huo.
Wifi huyo, Mary
Sambeke aliumwa na nyuki mwili mzima na kulazimika kuvua nguo zote hadharani na
baadaye alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC ambako aliongezewa maji
ya dawa(drip) ili kuokoa maisha yake.
Majeruhi wengine nane
walilazwa katika Hospitali ya Misheni ya Kibosho ambako walipatiwa huduma ya
kwanza na kisha kuruhusiwa kurudi nyumbani.
“Marehemu aliacha
usia kutokana na ndugu wa marehemu mumewe kukataa kuchangia matibabu yake
wakati akiwa hospitali , basi wasije wakajidai kuandaa sherehe wakati akifa kwa
kupika vyakula na vinywaji si mnaona shughuli ya kumzika imekwenda vizuri ila
kabla watu hawajala ndio nyuki wakajitokeza ?
”alisema mmoja wa ndugu wa
marehemu ambaye hakutaka jina lake litaandikwe gazetini
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa halmashauri ya Moshi Vijijini ambaye pia ni diwani wa kata ya
Ukaoni, Morris Makoyi akizungumzia tukio
hilo alisema ni mara ya kwanza kuona tukio la namna hiyo na limemshtua mno.
“Tulilazimika
kukimbia mbio kuokoa maisha yetu,ni tukio la kushangaza sana nyuki wengi kiasi
kile kutokea kusikojulikana na kuanza kushambulia waombolezaji kabla ya
kumaliza shughuli za mazishi”
“Kuna tetesi na madai
kuwa marehemu hakutaka chakula wala vinywaji wakati wa mazishi yake vitu
ambavyo gharama zake zingetosha kumtibu
ugonjwa uliomwua sasa sina hakika kama ni kweli,”alisema Mwenyekiti huyo
anayedaiwa kutaka kumng’oa Dk Cyril Chami katika nafasi ya ubunge katika
uchaguzi mkuu ujao jimbo la Moshi Vijijini.
Kaka wa marehemu
aliyefahamika kwa jina la Peter Mwacha inasemekana alilazimika kuwa dereva wa
bandarini kutokana na kuyasogeza magari ya waombolezaji zaidi ya 50
kwa umbali wa mita kadhaa kutoka msibani kutokana na wenye magari hao
kutawanyika ovyo kukimbia nyuki hao
Mmoja wa waombolezaji
aliyejitambulisha kwa jina la Temba aliwalaumu ndugu wa marehemu kwa kukiuka
usia marehemu ambaye aliweka bayana kwamba asingependa sherehe na madoido ya
aina yoyote katika msiba wake.
“Kabla na wakati wa mazishi nilikuwa
nikikumbusha alichosema marehemu lakini hawakutaka kusikia sasa matokeo yake
ndio haya, “alisisitiza Temba
Wakizungumzia tukio
hilo baadhi ya waombolezaji walishauri jamii kubadili mtizamo wake kwa
kuchangia mambo ya msingi kama kuwachangia wagonjwa katika matibabu badala ya
kutoa michango mikubwa pindi mgonjwa anapofariki.
“Lazima tubadilike
badala ya kuchanga mamilioni kwenye mazishi tuchange kumnusuru mgonjwa ili yeye
mwenyewe atambue mchango ule badala ya kuchangia maiti”alisema mmoja wa
waombolezaji ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini.
Tofauti na
wengine,Watanzania wamekuwa wepesi kutoa michango mikubwa katika shughuli za
sherehe na misiba badala ya kuwachangia wagonjwa na wanafunzi wa shule au vyuo kama wanavyofanya Kenya na Uganda na nchi
zingine.
ends
No comments:
Post a Comment