Na Mwandishi wetu
JAMAL Emil Malinzi, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Kagera (KRFA),
anatarajiwa kuchukua fomu ya kugombea Urais wa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) leo mchana, makao makuu ya shirikisho hilo, Ilala mjini Dar es
Salaam.
Habari ambazo BLOGU hii imezipata kutoka kwa
watu wa karibu wa Katibu huyo wa zamani wa klabu ya Yanga, zimesema kwamba
Malinzi atachukua fomu mchana wa leo.
Katika uchaguzi uliopita wa TFF uliofanyika Desemba 14, mwaka
2008, Malinzi alikuwa mpinzani mkuu wa rais anayemaliza muda wake, Leodegar
Chillah Tenga ambaye amekwishatangaza hagombei tena.
Katika uchaguzi huo, uliofanyika kwenye ukumbi wa NSSF Water
Front, Dar es Salaam, Tenga alishinda kwa kura 64 kwa 39.
Awali, Malinzi alienguliwa kwa kigezo cha uzoefu, lakini
akarejeshwa kuwania nafasi hiyo baada ya kushinda rufaa yake.
Katika uchaguzi huo ulioshuhudiwa na Mwakilishi wa FIFA,
Ashford Mamelodi, Athumani Nyamlani alishinda nafasi ya Makamu wa Kwanza wa
Rais, baada ya kujikusanyia kura 65 kati ya kura 107 zilizopigwa na kura mbili
kuharibika, akimshinda Lawrence Mwalusako aliyepata kura 39 na Ali Mwanakatwe
aliyeambulia kura moja.
Nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais, ambayo kwa sasa imefutwa, ilikwenda
kwa Ramadhani Nassib aliyemwangusha mpinzani wake wa karibu, Damas Ndumbaro
aliyepata kura 45.
Hadi sasa, mbali na Malinzi mgombea mwingine anayetarajiwa
katika nafasi ya Urais ni Athumani Nyamlani, Makamu wa kwanza wa sasa wa Rais
wa TFF.
Jumla ya watu 26 hadi jana walikuwa wamekwishachukua fomu za
kugombea nafasi mbalimbali, kuelekea uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Februari
24, mwaka huu.
Hata hivyo, idadi hiyo ni kwa wale wanaochukua fomu hizo
katika ofisi za TFF, kwani vilevile zinapatikana kupitia tovuti ya TFF ya
www.tff.or.tz ambapo mwisho wa kuchukua na kurejesha ni saa 10 kamili alasiri
Januari 18 mwaka huu.
Waliochukua jana ni Michael Wambura anayewania umakamu wa
rais wakati kwa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni Mbasha Matutu, Muhsin
Balhabou, Salum Chama, Titus Osoro na Zafarani Damoder.
Idadi kamili ya waliochukua ni Michael Wambura, Ramadhan
Nassib na Wallace Karia (Makamu wa Rais). Kwa upande wa wajumbe na kanda zao
kwenye mabano ni Salum Chama (Kagera na Geita), Mugisha Galibona, Samuel
Nyalla, Titus Osoro na Vedastus Lufano (Mara na Mwanza).
Epaphra Swai na Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu), Charles
Mugondo, Elly Mbise na Twahili Njoki (Arusha na Manyara), Yusuph Kitumbo
(Kigoma na Tabora), Ayubu Nyaulingo, Nazarius Kilungeja na Selemani Kameya
(Katavi na Rukwa) na James Mhagama (Njombe na Ruvuma).
Athuman Kambi (Lindi na Mtwara), Hussein Mwamba na Stewart
Masima (Dodoma na Singida), Farid Nahdi (Morogoro na Pwani), Khalid Mohamed
(Kilimanjaro na Tanga) na Muhsin Balhabou, Shaffih Dauda na Zafarani Damoder
(Dar es Salaam).
Mwenyekiti wa soka wa Kagera, Jamal Malinzi kushoto katika picha ya pamoja na Rais wa TFF anayeng'atuka katika nafasi hiyo Leodigar Tenga |
No comments:
Post a Comment