Na: Mwandishi wetu, Morogoro
Katika
kupambana na wimbi la kupunguza umaskini hapa nchini,Kampuni ya
Mawasiliano ya Vodacom Tanzania kupitia mradi wake wa kuwakopesha
wanawake wajasiriamali wadogo ujulikanao kama M-Pesa Women Empowerment
Initiative (MWEI),imewakopesha wanawake wajasiriamali wadogo zaidi ya
150 wa kijiji cha Luhembe wilaya ya
Kilosa Mkoani Morogoro, wamepatiwa mkopo huo usio na riba wa zaidi ya shilingi Milioni tisa.
Wanawake
hao waliodai kutumia fedha hizo kuboresha mitaji yao kibiashara ili
kujikwamua na umaskini, walisema hii ni mara ya kwanza kupata mkopo wa
aina hiyo wenye masharti nafuu, ambapo wanalipa kiasi kile kile cha
fedha ambacho wanakuwa wamekopa.
Baadhi ya wanawake hao wenye mitaji ya kuanzia shilingi elfu tano
hadi laki moja walionufaika na mikopo midogo midogo kupitia MWEI,
walisema wataweza kutumia mikopo hiyo kukuza biashara zao, sambamba na
kubuni biashara mpya kuendana na mazingira yaliyopo ili waweze kuzalisha
zaidi na kulipa mikopo hiyo kwa wakati.Akizungumzia mkopo huo, Meneja wa Vodacom Foundation, Grace Lyon,alisema Mradi huo ulioanza miaka mitatu iliyopita unalenga kuwasaidia wanawake wajasiriamali wadogo wadogo vijijini kwa kutumia njia ya M-PESA, na kwamba tayari wameshavifikia vijiji 42 hapa nchini, huku mkoa wa Morogoro Luhembe kikiwa ni kijiji cha nne, vingine vikiwa ni Mkuyuni, Kimamba na Mkamba.
Meneja huyo alisema mama ndiye kichwa cha familia, hivyo kumuwezesha mwanamke ni kuiwezesha jamii nzima,pia alitumia frusa hiyo ya kuwaasa wakina mama hao kutumia mikopo wanayopewa kwa shughuli za maendeleo ili waweze kurejesha mikopo hiyo kwani masharti ni nafuu na mwezi wa kwanza unatakiwa kutumia kwa ajili ya biashara na mwezi unaofuata utakuwa kulipa nusu ya fedha waliyokopeshwa na nusu nyingine kumalizia mwezi mwingine bila riba yeyote.
Alisisitiza mkopo huo unalenga kuimarisha biashara na sio kufungua biashara mpya, na kuwahimiza kurudisha marejesho ili waweze kupata mkopo mara mbili zaidi ya waliochukua awali.
Akizindua mikopo hiyo, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mkuu wa wilaya ya Kilosa, Elias Tarimo aliipongeza Vodacom kwa hatua hiyo ya kulenga kupunguza umaskini kwa kinamama wajasiriamali, ambapo kitendo wanachofanya ni kuunga mkono jitihada za Serikali za kupambana na umaskini.
Aliwaasa wakina mama wanaofaidika na mikopo hiyo kutambua masharti ya mikopo, ikiwemo kuhakikisha wanarudisha fedha walizokopa baada ya kuzalisha, ili fedha inayopatikana iweze kusaidia wanawake wengine wenye mahitaji zaidi kama wao na kujenga uaminifu wa kujiongezea kupata mikopo zaidi ya awali.
“Hii ni fursa nzuri kwenu ya kuondokana na umaskini, mikopo ndio chombo pekee cha kuweza kutukwamua na umaskini, muhimu ni kujipanga ujue unawekeza wapi, shughuli gani, ili mwisho wa siku uweze kurudisha mkopo na kupata ziada ya kuendeleza biashara zako, jitahidini mfike mahali msimame wenyewe na hatimaye kuendesha vyema maisha yenu”Alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Kwa upande wake Richard Kigave, afisa mtendaji kata ya Luhembe,aliwaasa mikopo waliyopewa waitumie kwa malengo yaliyokusudiwa na iwapo watakiuka kulipa kwa wakati, wataishia kwenye mkono wa sheria.
“Inaonekana Vodacom walitizama wana Luhembe wakaona kweli tuna shida kubwa na hali ngumu hivyo tunahitaji kujikwamua na umaskini na wakaamua kutuletea hii mikopo,sasa sitegemei kupokea mgogoro wowote unaohusu ninyi na kampuni hii iliyokuja kwa nia njema”Alisema Mtendaji huyo wa kata.
PICHA NA HABARI KWA NIABA YA MJENGWABLOG
No comments:
Post a Comment