SPIKA wa Bunge, Anne Makinda ametangaza mabadiliko ya Kamati za Kudumu za Bunge, huku Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ikifutwa.
Kutokana na mabadiliko hayo, shughuli za
POAC sasa zitaendelea kufanywa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC),
ambayo itaendelea na jukumu lake la msingi la kuchambua taarifa ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kwa Serikaki
Kuu.
Kamati nyingine iliyofutwa ni ya sheria ndogo, huku Spika akiunda kamati mpya tatu na nyingine kuzifanyia marekebisho kadhaa ikiwa ni hatua ya kuimarisha usimamizi wa Bunge kwa shughuli za Serikali.
Akitangaza mabadiliko hayo muda mfupi kabla ya kuahirisha mkutano wa kumi jana, Makinda alizitaja kamati mpya kuwa ni Kamati ya Bajeti, Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Kamati ya Ulinzi na Usalama, ambayo imetenganishwa kutoka Kamati ya kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.
Kwa mujibu wa Spika Makinda majukumu ya kamati mpya ya bajeti ni kufuatalia utekelezaji wa Bajeti ya Serikali, Sera za Fedha, kuanisha na kupendekeza vyanzo vya mapato ya Serikali na kufuatilia mwenendo wa uchumi.
Kamati hiyo pia imepewa jukumu la kushauri kamati nyingine zote kuhusu bajeti.
“Kwa sasa kuna baadhi ya kamati zinazosimamia wizara moja moja, ambazo shughuli zake siyo nyingi ikilinganishwa na kamati nyingine zinazosimamia wizara zaidi ya moja zikiwa na shughuli nyingi,”alisema Makinda na kuongeza:
“Vivyo hivyo kuna wizara zinazohusika na kutunga sera, lakini kwa kiasi kikubwa sera hizo zinatekelezwa na wizara nyingine hadi ngazi za chini. Mfumo huu husababisha baadhi ya Kamati za Bunge kutoweza kufuatilia vizuri utekelezaji wa shughuli za Serikali, kinyume na matakwa ya ibara ya 63(3) ya Katiba na majukumu ya kamati yaliyoainishwa na Kanuni za Bunge.”
Spika alifanya marekebisho hayo kwa mamlaka aliyopewa kwa kanuni ya 152 (3) cha Kanuni za kudumu za Bunge toleo la 2007.
Kamati ambazo zimebadilishwa miundo yake ni ya Katiba, Sheria na Utawala, Fedha na Uchumi, Viwanda na Biashara na Kamati ya Masuala ya Ukimwi.
Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara imeundwa na imepewa wajibu wa kusimamia masuala ya uchumi, mitaji, uwekezaji, maendeleo ya viwanda na shughuli za biashara.
Makinda alisema Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, imepunguziwa majukumu na sasa itajikita kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na taasisi zake na Wizara ya Katiba na Sheria.
“Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa itasimamia utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), pamoja na sheria ndogo za halmashauri zote nchini,”alisema Makinda.
Alisema kwamba jukumu la Kamati ya Huduma za Jamii ni kufuatilia utekelezaji wa Wizara ya Elimu na Mfunzo ya Ufundi kwa ngazi ya elimu ya Juu, Vyuo vya Ualimu, Elimu ya Ufundi (Veta) na taasisi za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Pia Vyuo vya Elimu ya Juu vya Umma, Baraza la Mitihani, Taasisi ya Kukuza Mitaala na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Kamati hiyo pia itasimamia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Spika alilieleza Bunge kuwa Kamati Nyingine ni ya Ukimwi na Dawa za kulevya, ambayo imeongezewa jukumu la kufuatilia masuala ya matumizi ya dawa hizo.
No comments:
Post a Comment