DHAMBI iliyoachwa kwa
muda mrefu bila kukemewa ni matokeo ya majanga yanayoikabili Tanzania hivi sasa
na kusababisha mauaji ya watumishi wa dini ya Kikristo nchini, kufeli kwa
wanafunzi kidato cha nne, mvua kutonyesha kwa wakati.
Hayo yalielezwa jana
jijini hapa na mchungaji Jovin Msuya wa huduma ya redio safina alipokuwa
akihubiri kwenye kongamano maalum la kuiombea Taifa kuondokana na majanga hayo.
Mchungaji Msuya alisema
matokeo ya dhambi hiyo ni vuguvugu la uvunjifu wa amani na utulivu ambao
umejitokeza hivi sasa nchini na kwamba endapo waumini wa dini mbalimbali nchini
hawatajitokeza kukemea matokeo yake ya baadae ni makubwa zaidi.
“Ili kutokomeza dhambi
hizi ni wakati muafaka sasa kwa mamlaka za Kiserikali kwa kushirikiana na
viongozi, taasisi na waumini wa dini zote nchini kutumia mamlaka walizokuwa
nazo kukemea na kupatia suluhu vurugu ambazo zimekuwa zikitokea ili kurejesha
amani na utulivu ulioanza kutoweka,”alisema
Msuya.
Aliwataka watanzania wa
dini mbalimbali kuacha vurugu na uchochezi ndani ya nchi na badala yake
kuhamasisha maombi ya kukemea roho za umauti
ambazo matokeo yake ni mauaji ya viongozi.
Alisema kila jambo ambalo limekuwa likitokea nchini
limekuwa na sababu yake kwa Mungu hivyo kuwataka watanzania kujiuliza sababu iliyopelekea
kufeli kwa wanafunzi wahitimu wa kidato cha nne sanjari na mauaji ya viongozi wa dini.
Aidha Mchungaji
Christian Mwabukusi, alisema maovu mengi ambayo yamekuwa yakitokea ndani ya
jamii yamekuwa yakichangiwa na ugumu wa maisha waliyokuwa nayo watanzania
kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa ajira.
Alisema maombezi kwa
Taifa yanayofanywa na redio hiyo yatakuwa yakifanyika mara moja kila baada ya
miezi mitatu na kutoa wito kwa watanzania kuungana katika maombi hayo ili
kunusuru Taifa katika dhambi.
No comments:
Post a Comment