ARUSHA
WAZIRI wa katiba na sheria Mathias
Chikawe ameitaka tume ya mabadiliko ya katiba kuwatumia kikamilifu
Majaji,mahakimu,Mawakili na wanasheria kote nchini katika mchakato wa
mabadiliko ya katiba kwakua ni watumiaji wakubwa wa katiba ya sasa.
Chikawe ametoa changamoto hiyo leo
alipokua akifungua warsha ya siku moja inayoendelea katika hoteli ya kitalii ya
Snow Crest jijini Arusha ya umuhimu wa katiba katika utoaji wa haki katika
vyombo vya maamuzi ikiwemo mahakama.
Warsha hiyo ambayo imeungana na
mkutano wa mwaka wa majaji na mahakimu wa mahakama zote hapa nchini ukiwa na
lengo la kutazama namna haki inavyoweza kupatikana na kwa wakati katika vyombo
mbalimbali vya kutafsiri sheria za nchi.
Waziri Chikawe alisema mchango wa
majaji,mahakimu na mawakili unatokana na ukweli kwamba kundi hilo linatafsiri
za kuzibadili kila siku sheria mbalimbali za nchi zinazotokana na katiba hali
ambayo inaweza kutoa mchango mkubwa kwa tume hiyo ya mabadiliko ya katiba
ya nchi.
“hili kundi ni muhimu sana kwakua wao
ndiyo kazi yao kila siku wanapotoa hukumu au utetezi wanatafsiri sheria ambazo
nyingi zipo ndani ya katiba ambayo ndiyo sheria mama baada ya kuziona kama zina
mapungufu ikiwemo kupitwa na wakati”alisema Chikawe.
Hata hivyo Chikawe alisema kwasasa
wizara yake imejipanga kikamilifu katika kuhakikisha haki inapatikana kwa
wakati bila kucheleweshwa ikiwa ni kwa kuboresha uendeshaji wa mashauri
mbalimbali yaliyopo katika mahakama zote nchini.
Alisema uboreshaji huo ni pamoja na
kuachana na matumizi ya majaji na mahakimu kuandika mashauri kwa kutumia mkono
na badala yake waanze kutumia njia mbadala zikiwemo za kielektroniki ili
kurahisisha kazi zao.
Alisema kufanikiwa kuondokana na
teknolojia hiyo ya kizamani kutawezesha kupunguza msongamano wa mashauri katika
mahakama hapa nchini ambapo wananchi wengi hufikia hatua ya kukosa imani na
chombo hicho na kutafuta njia za mkato katika kutafuta haki zao ambazo ni
pamoja na kutoa rushwa.
Hata hivyo aliahidi kufanyiwa kazi
kwa marekebisho mbalimbali ya sheria No.4 ya mwaka 2012 ambayo inataka
kutenganishwa kwa shughuli za kimahakama na za kiutendaji wa
serikali,kuanzishwa kwa mfuko wa mahakama pamoja na kurejeshwa kwa uwajibikaji
wa watumishi kwa kuwaweka chini ya idara ya mahakama.
Pia aliwataka wakuu wa vyombo hivyo
kuwa wakali kwa wale wote wanaoonekana kuichafua sekta hiyo kwa kufanya kazi
kinyume na maadili ikiwa ni pamoja na kuwafukuza kazi pasipo kuwaonea haya ili
kubaki na wale wanaofanya kazi hiyo kwa wito kama inavyotakiwa.
Mkutano pamoja na warsha hiyo
inahudhuriwa na viongozi wa ngazi zote za mahakama kutoka Tanzania bara na
Zanzibar pamoja na nchi jirani ikiwemo Kenya kwaajili ya kubadilishana uzoefu
wa masuala ya kisheria.
No comments:
Post a Comment