Monday, 5 November 2012

Makatibu wakuu wazee wadaiwa kupiga hodi Ikulu, kuomba mwaka



Ikulu ya Tanzania

Makatibu wakuu wazee wadaiwa kupiga hodi Ikulu, kuomba mwaka


KAULI ya Katibu Mkuu Kiongozi, 0mbeni Sefue kuwataka Makatibu Wakuu wa Wizara wenye umri wa zaidi ya  miaka 60 waachie ngazi  imewatetemesha wahusika huku wengine wakidaiwa kukimbilia Ikulu kuomba waongezewe muda wa mwaka mmoja.
Hivi karibuni Ombeni alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema makatibu wakuu wenye umri mkubwa waondoke kutokana na ukweli kwamba wapo wafanyakazi wengi wazuri.

Hata hivyo alisema yeye hana mamlaka ya kuwaondoa kwani mwenye mamlaka ni yule aliyewateua ambaye ni Rais.

Kufuatia kauli hiyo, habari za uhakika zimesema Makatibu Wakuu  wawili (majina yanahifadhiwa) ,wamewasilisha barua Ikulu kuomba kuongezewa muda  wa walau mwaka mmoja kwa maelezo kwamba  wana mambo wanayotaka kuyamalizia  katika Wizara husika.
Barua hizo waliziwasilisha wakati Rais akiwa safari za nje hivi karibuni na kwamba hatua hiyo ilifikiwa baada ya kufanya kikao cha siri kwenye hoteli moja ambapo waliijadili kwa kina taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi.
Ofisa kutoka Ofisi ya Rais Utumishi ambaye jina lake linahifadhiwa alisema kwa mujibu wa kanuni za utumishi, mfanyakazi yeyote wa umma anatakiwa kustaafu  kwa hiari akiwa na miaka 55, lakini kwa lazima ni miaka 60.
Alisema kitendo cha wafanyakazi wa umma kufanya kazi zaidi ya umri huo ni kukiuka taratibu za utumishi na hata katiba ya nchi.
Habari zilisema kwa mara ya mwisho makatibu wakuu  hao walifikisha umri wa miaka 60 mwaka juzi, lakini waliomba kuongezewa miaka miwili ambayo wamemaliza na sasa wameomba tena mwaka mmoja.

“Makatibu wakuu  wanaoomba muda zaidi hawaitakii mema Serikali, kwani wapo walioomba muda huo na ghafla waliibuka na utajiri wa kutisha kwa kujenga maghorofa, hoteli kubwa ndani na nje ya nchi’,’alisema   Ofisa kutokaWizara ya Ujenzi.
Alisema zipo taarifa za baadhi ya makatibu  wakuu kuwa na mitandano ya ufisadi huku wengine wakituhumiwa kupenda kupanga upya wakurugenzi  wa idara kwa nia ya kufanikisha mipango ya ufisadi.

Mmoja wa makatibu wakuu hao mapema mwaka huu alitoa dokezo kwenye wizara yake kwamba anastaafu , lakini ghafla alibadili msimamo na sasa amekataa hata kukabidhi ofisi yake wakati akienda kwenye likizo ya kawaida.
Habari zilisema nia yao kubwa ni kutaka kustaafu  sawa na Serikali ya Awamu ya Nne mwaka 2015.

No comments:

Post a Comment