Madaktari wamethibitisha afya yangu ni njema- Lowassa
Na Mwandishi Wetu
Waziri Mkuu (mstaafu), Edward Lowassa, amezungumzia afya yake na kueleza kwamba madaktari waliomfanyia uchunguzi wa vipimo wamethibitisha kwamba ni njema.
Taarifa ya Lowassa ambaye pia ni mbunge wa
Monduli (CCM), kwa vyombo vya habari jana ilieleza kwamba kutokana na
afya yake kuwa nzuri atarejea nchini kutoka Munich, Ujerumani hivi
karibuni.
“Namshukuru Mungu siha yangu ni imara na
kwamba madaktari walionifanyia uchunguzi wamejiridhisha pasi na shaka
kwamba afya yangu ni njema…nimeendelea kupata maendeleo na matibabu
mazuri katika jicho langu moja ambalo nilifanyiwa upasuaji miaka miwili
iliyopita hapa hapa, Ujerumani,” alisema katika taarifa hiyo.
Alisema “natarajia kurejea nyumbani wakati
wowote kuanzia sasa ili kuja kuungana na Watanzania wenzangu katika
kulijenga taifa letu.”
Alisema amekuwa jijini Munich kwa wiki
nzima sasa na kwamba amekuwa akifuatilia kwa karibu taarifa mbalimbali
za kisiasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi na katika taifa kwa ujumla.
“Nikiwa mwana CCM na Mtanzania
nasononeshwa sana na taarifa za kukithiri kwa vitendo vya rushwa ndani
ya chama chetu, serikalini na katika taasisi mbalimbali,” alisema.
Alisema rushwa ni tatizo na kansa ambayo
inapaswa kutafutiwa ufumbuzi wa kimfumo badala ya kuendelea kufikiri
kwamba linaweza kumalizwa kwa njia ya kulalamika, kulaumiana na kupakana
matope.
Alisema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru), inatakiwa kupewa meno na kuimarishwa zaidi katika
kukabiliana na vitendo hivyo na kwamba rushwa inahitaji mikakati mipana
zaidi na mijadala wa kitaifa na ya kina katika kukabiliana nayo.
No comments:
Post a Comment